KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Friday 27 February 2015

AFA KWA KUNG'ATWA NA PAKA



MKAZI wa Gongolamboto, wilayani Ilala, Dar es Salaam, Simon Chibago, amefariki dunia baada ya kung’atwa na paka aliyekuwa akimfuga nyumbani kwake.
Akizungumza na BLOGG hiileo, mmoja wa ndugu wa marehemu, Rajabu Mustafa, alisema tukio la ndugu yao kung’atwa na paka lilitokea Februari  14, mwaka huu.
“Chibago alikuwa ana paka mmoja aliyekuwa anamfuga nyumbani kwake, siku hiyo aliporudi nyumbani alimuona paka akihangaika na kumfuata miguuni akionyesha kuomba msaada, ndipo alipodhani amepewa sumu, hivyo akaenda kununua maziwa ili ampe,” alisema Mustafa.
Alisema Chibago aling’atwa kwenye kidole cha mkono na paka huyo baada ya kutaka kumpa maziwa.
Mustafa alisema baada ya kung’atwa, Chibago hakwenda hospitali kupata tiba, bali aliendelea na kazi zake kama kawaida huku akishindwa kuwaeleza ndugu zake hadi hali ilipoanza kuwa mbaya.
“Chibago alianza kupata maumivu makali, hali iliyowafanya siku ya Jumamosi Februari 21, mwaka huu kumpeleka Hospitali ya Amana na baadaye kuhamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa uchunguzi zaidi,” alisema Mustafa.
Mustafa alisema hata hivyo Jumatatu ya Februari 23, alifariki  dunia na walielezwa chanzo cha kifo ni sumu ya paka huyo iliyosambaa mwilini  kutokana na kuchelewa kutibu jeraha hilo.
Alisema Chibago alizikwa juzi Alhamisi. Paka huyo pia alikufa siku aliyomng’ata Chibago.

No comments:

Post a Comment