NA BASHIRU ALLY
Kuna kila dalili kwamba baadhi ya Asasi za Kiraia (AZAKI)
zinazoendesha shughuli zake katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC) zimeanza kushiriki katika mjadala juu ya namna bora na endelevu
ya utekelezaji wa wazo la kuundwa kwa soko la pamoja (common market) la Afrika
Mashariki.
Makala haya yanadadisi kwa muhtasari mwelekeo wa
mjadala huo na athari zake kwa maendeleo endelevu ya EAC.
Makala haya yanaainisha pia masuala ya msingi
yanayojadiliwa. Moja ya hoja nzito za mjadala huo ni kwamba kuundwa kwa soko la
pamoja hakutakuwa na tija ikiwa uchumi wa nchi za EAC utaendelea kuwa duni na
tegemezi.
Hii ni hoja nzito inayotakiwa kuchambuliwa kwa undani.
Makala haya yanajaribu kufanya hivyo.
Watoaji wa hoja hiyo wanadai kuwa uchumi duni na tegemezi ni
miongoni mwa vikwazo vikuu vya utekelezaji endelevu wa malengo ya EAC.
Wanadai kuwa bila kuwa na mfumo mbadala wa kisiasa na
kiuchumi katika nchi wananchama wa EAC, soko la pamoja halitakuwa na manufaa
kwa wananchi wengi, hasa wavujajasho, kwani matunda yake yatavunwa na wajanja
wachache wenye uwezo wa kifedha na madaraka ya kisiasa.
Katika muktadha huu, jukumu kubwa la AZAKI ni kuchambua kwa
undani hoja hii na hatimaye kubuni mbinu mbadala za kujenga mshikamano wa
wavujajasho ili waweze kunufaika na matunda ya EAC.
Hoja iliyoainishwa hapo juu msingi wake ni historia ya
ubeberu (imperialism) na pia muktadha wa sasa wa utandawazi wa kibepari
(capitalist globalisation).
Kwa sababu za kihistoria, EAC ni chombo ambacho kimejengwa
juu ya mfumo kandamizi wa ubepari wa kibeberu (imperialist capitalism)
unaodhibitiwa na dola kuu za kibeberu hasa Marekani, Uingereza, Ujerumani na
Ufaransa kwa kushirikiana na mashirika ya kimataifa ya fedha na biashara yaani
Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Biashara
Duniani (WTO).
Ubeberu wa kibepari (imperialist capitalism) ulizaliwa Ulaya
Magharibi katika karne ya 18 na baadaye kuenezwa kimabavu na kikatili katika
nchi za Afrika kwa mtindo wa ukoloni. Historia hii ndiyo kiini cha kudidimia
kwa uchumi katika nchi zote za JAM.
Hata baada ya miaka zaidi ya hamsini ya uhuru wa bendera
(flag independence), dola kuu za kibeberu zimeendelea kudidimiza maendeleo ya
nchi wanachama wa EAC kwa njia na mbinu za kijeshi, biashara, mikopo, misaada,
teknolojia, siasa, diplomasia na uwekezaji.
Ndiyo maana hadi sasa uchumi wa nchi za EAC ni duni na
tegemezi kwa nchi za kibeberu. Kwa mfano, sekta ya viwanda katika nchi hizo ni dhaifu na mchango wake kiuchumi ni
mdogo.
Kwa kiwango
kikubwa uchumi wa nchi hizi bado unategemea zaidi uuzwaji nje wa bidhaa ghafi
za kilimo na madini.
Vile vile
biashara ya nje inachukua nafasi kubwa na ya kipekee katika uchumi mzima
kwa sababu sekta ya uchuuzi na hasa uchuuzi wa bidhaa zilizoagizwa kutoka nje
ndiyo unaochangamkiwa zaidi na wajasiriamali kwa sababu ya uhakika wa kuchuma
faida kwa haraka.
Hata hivyo,
uchuuzi unachangia kuua viwanda vya nchi za EAC na hivyo kupoteza fursa za
ajira na mapato ya serikali.
Uchuuzi unaua pia
ari ya uzalishaji wa chakula na bidhaa nyingine muhimu kwa mahitaji ya wakazi
wa nchi wanachama wa EAC.
Vilevile, vitega uchumi
vingi vinaelekezwa katika sekta za fedha, nyumba, mawasiliano, madini na
uchuuzi wa bidhaa za anasa. Hizi ndizo sekta zinazowavutia zaidi wawekezaji wa
nje na ndani kwa sababu kuna fursa za kuchuma faida kwa mtindo wa ’fastafasta’.
Jambo baya zaidi
ni kwamba sehemu kubwa ya faida inayochumwa na wawekezaji wa nje inalimbikizwa
nje ya nchi za EAC.
Bila shaka,
wawekezaji wakubwa kutoka nje siyo ’wakombozi’ wala 'wabia wa maendeleo’ kwani
kipaumbele chao ni kuvuna faida nono na siyo kuleta maendeleo endelevu ya nchi
za JAM.
Hata mitaji ya
wananchi wa nchi za EAC haifui dafu kwa mitaji ya wawekezaji kutoka nje.
Matokeo yake wawekezaji raia katika nchi za JAM wanalazimika kuwa mawakala au
wabia wadogo wa wawekezaji wa nje.
Kwa kiwango
kikubwa, utegemezi wa mitaji kutoka nje ni kikwazo cha maendeleo endelevu
katika nchi za EAC.
Hata wazalishaji
wadogo katika sekta za kilimo, uvuvi, madini, mifugo na viwanda hawanufaiki na
jasho lao na hata mazingira yao ya uzalishaji ni duni.
Katika hali hiyo,
wenye mitaji mikubwa wanatumia hila kuwanyonya wazalishaji wadogo kwa kutumia
mbinu chafu za kibiashara, mikopo, bei za pembejeo na bei za bidhaa na huduma
muhimu kama vile elimu, nyumba, nishati na afya.
Unyonyaji wa aina
hii unawezeshwa na sheria mbovu zinazotungwa na kusimamiwa na watumishi wa umma
na wanasiasa ambao wanashinikizwa na taasisi za kimataifa za kibeberu.
Ndoto za kuundwa, hatua kwa hatua, kwa Shirikisho la Afrika
Mashariki haziwezi kutimia ikiwa muundo wa uchumi katika nchi wanachama wa EAC
utaendelea kuwa na sifa zilizoainishwa hapo juu.
Hivi sasa hakuna dalili kwamba malengo na mikakati ya
kiuchumi katika EAC yanaongozwa na dira ya ukombozi kama ilivyokuwa enzi za
mapambano dhidi ya ukoloni na ukaburu.
Mapambano ya ukombozi wa kiuchumi yametelekezwa.
Hata hoja nyingi za mjadala uliopo sasa juu ya mwelekeo wa
EAC hazikosoi mfumo unaotamalaki sasa wa utandawazi wa kibepari ingawa mfumo
huu ndio kikwazo kikuu cha maendeleo ya nchi wanachama wa EAC.
Mfumo wa utandawazi wa kibepari ni kikwazo kwa sababu
uchumi wa nchi wanachama wa EAC unaendelea kuwa chini ya himaya ya nchi za
kibeberu.
Kwa hiyo, hoja kuu siyo hofu au shauku ya kuundwa kwa soko
la pamoja la EAC bali ni mwelekeo tenge wa maendeleo ya nchi wanachama wa EAC
na hasa namna nchi hizo zinavyoshindwa kusimamia na kuongoza mchakato wa
mageuzi ya mifumo yao ya kiuchumi na kisiasa kwa maslahi ya wananchi wake.
Katika muktadha
wa utandawazi wa kibepari, nchi wanachama wa EAC zinatakiwa kuwa na mikakati ya
mageuzi katika mifumo yao ya kisiasa na kiuchumi inayowiana na inayooongozwa na
dira ya ukombozi wa wavuja jasho.
Katika harakati
za ukombozi wa kiuchumi, maendeleo ya kasi katika sekta za elimu, afya, maji,
nishati, madini, fedha na mawasiliano yanahitajika.
Bila shaka
uwekezaji wa pamoja baina ya nchi wanachama wa EAC utahitajika ili utekelezaji
wa mikakati ya aina hiyo uwe wa ufanisi na endelevu.
Hii ina maana
kwamba masoko ya fedha, bidhaa na ajira yatakuwa chini ya uratibu wa EAC na
hatimaye kujenga msingi imara wa kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki.
Vile vile, sekta
nyeti kiuchumi hasa fedha, mawasiliano, madini, nishati na viwanda zinatakiwa
kumilikiwa na wananchi wa nchi wanachama wa EAC.
Mageuzi ya
kiuchumi na kisiasa ya aina hii yanaweza kuanzisha safari ndefu ya kuelekea
kwenye ujenzi wa ujamaa wa soko (market socialism) na demokrasia ya
wavujajasho (popular democracy).
Kwa maoni yangu, huu ndiyo mkakati
mbadala wa kuziondoa nchi wanachama wa EAC katika makucha ya dola kuu za
kibeberu na vibaraka wao. Hata hivyo, haya yote hayawezi kutokea ikiwa ushiriki
wa wavujajasho katika uendeshaji wa uchumi na siasa katika nchi wanachama wa
EAC utakuwa mdogo kama ilivyo sasa.
Kwa hiyo,
kazi kubwa ya AZAKI ni kuhamasisha wavujajasho wa nchi zote wanachama wa EAC
kudai mfumo mbadala wa siasa, uchumi wenye manufaa kwa uhuru, haki na utu wao.
Hata AZAKI
zenyewe zinatakiwa kukataa katakata fadhila fedheheshi za mabeberu na vibaraka
wao.
(Mwandishi wa
Makala haya ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)
akifafanua kwa undani sehemu ya Mada aliyoiwasilisha kwenye Kongamano la AZAKI
juu ya Mtangamano wa Afrika ya Mashariki lililoandaliwa na Foundation for Civil
Society (FCS) Desemba 2014, jijini Arusha.)
No comments:
Post a Comment