SERIKALI imesema inaandaa mswada
wa sheria ambayo itawalinda watoaji wa taarifa za masuala ya uhalifu
ikiwa ni jitihada za kuimarisha mapambano dhidi ya vitendo mbalimbali
vya uhalifu nchini Tanzania.
Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki
jijini Dar es Salaam na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. George Masaju
alipokuwa akitoa vyeti kwa baadhi ya waandishi wa habari waliokuwa
katika mpango wa kuandika habari za dawa za kulevya pamoja na mafanikio
na changamoto za mpango wa milenia.
Akizungumza katika hafla hiyo
iliyoandaliwa kwa ushirikiano na Umoja wa Mataifa (UN) na Mfuko wa
Wanahabari Tanzania (TMF), Masaju alisema kwa sasa ni Sheria ya Makosa
ya Rushwa (ufisadi) tu ndiyo inayowalinda watoaji wa taarifa hizo kwani
imekataza wao kutajwa tofauti katika maeneo mengine ya sheria.
Alisema katika sheria hiyo mpya
inayokusudiwa kutungwa na Serikali itapanua wigo wa ulinzi kwa watoaji
wa taarifa kutotajwa endapo watatoa taarifa juu ya makosa yoyote jambo
ambalo alisema litasaidia katika mapambano ya uhalifu.
“Serikali
inaandaa muswada wa Sheria ya kuwalinda watoa taarifa wa vitendo vya
uhalifu (whistle blowers protection bill) ili kuimarisha mapambano dhidi
ya uhalifu wa aina zozote nchini. Kwa sasa ni watoa taarifa wa makosa
ya rushwa (ufisadi) tu ndio wanatamkwa katika sheria ya kuzuia na
Kupambana na Rushwa, 2007 kulindwa wasitajwe,” alisema Mwanasheria Mkuu.
Aidha alisema Sheria mpya ya
Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya ya Mwaka 2015 ambayo imepitishwa
na Bunge hivi karibuni imetungwa kwa kuzingatia mapungufu ya sheria za
nyuma hivyo itakuwa na nguvu zaidi ya kupambana na uhalifu huo tofauti
na ilivyokuwa awali.
Alikiri kuwa sheria ya awali
ilikuwa na mapungufu kadhaa jambo ambalo lilichangia sheria hiyo
kushindwa kufanya kazi kikamilifu katika mapambano.
Alisema miongozi mwa
mapungufu kwa sheria iliyokuwa ikitumika awali ni pamoja na kutotoa
adhabu kulingana na ukubwa wa kosa, na haikuainisha masharti bora ya
udhibiti wa madawa ya kulevya kama ilivyo kwa sheria mpya.
Alisema sheria mpya imeanzisha
Baraza la Taifa la Kudhibiti Dawa za Kulevya ambapo mwenyekiti wake ni
Waziri Mkuu wa Tanzania na wajumbe wake watatoka pande zote za Muungano
yaani Tanzania Bara na Visiwani, alisema kazi kubwa ya balaza hilo ni
kusimamia utekelezaji wa Sera ya Udhibiti wa Dawa za kulevya.
“Sheria iliyopo ina udhaifu wa
adhabu, haitoi adhabu kulingana na ukubwa wa kosa kwenye baadhi ya
makosa, hivyo kusababisha kukosekana kwa mizania ya haki. Sheria mpya
imeweka kima cha kuanzia cha adhabu iwe ni faini au kifungo. …Mfano
sheria mpya imeweka adhabu ya faini isiyopungua milioni 50 na isiyozidi
milioni 500 au kifungo kisichopungua miaka 7 na kisichozidi miaka 30 au
vyote kwa pamoja.”
Alifafanua Masaju katika hotuba yake.
Jumla ya waandishi wa habari 18
walipata mafunzo ya namna ya kuripoti habari za dawa za kulevya pamoja
na kuripoti habari za malengo ya milenia baada ya kuwezeshwa na Shirika
la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP)kwa kushirikiana na mfuko wa
wanahabari Tanzania (TMF) na kukabidhiwa vyeti na mgeni rasmi,
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Masaju.
No comments:
Post a Comment