KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Friday 10 July 2015

KITUO CHA POLISI BUNJU CHA CHOMWA MOTO NA WANANCHI




JESHI la Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni linawashikilia watu watano kwa tuhuma za kuchoma kituo kidogo cha Polisi kilichopo Bunju ‘A’ jijini Dar es Salam.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Camillus Wambura alisema tukio hilo lilitokea saa 3:00 asubuhi leo, wakati Tanroads pamoja na Jeshi la Polisi walipokuwa katika mazungumzo ya kuweka matuta katika barabara hiyo.
Alisema kabla ya kuchomwa kituo hicho dereva aliyetambulika kwa jina la Yohana John aliyekuwa akiendesha gari aina ya Coaster alisababisha ajali katika eneo hilo na kumgonga mwanafunzi  mmoja wa shule ya Bunjua ‘A’  Radhia Omary na kusababisha kifo chake.
Wambura, lisema baada ya mwanafunzi huyo kupoteza maisha wanafunzi wa shule hiyo pamoja na wananchi wa eneo hilo walikusanyika na kulala  barabarani hali iliyosababaisha magari kutoendelea na safari zake.
Alisema wananchi hao pamoja na wanafunzi walifunga barabara hiyo kwa muda wa saa tatu wakidai kuwa wanataka matuta yawekwe katika eneo hilo lililopo karibu na shule hiyo ili liweze kuwasaidia wanafunzi wakati wa kuvuka barabara.
Hali hiyo ilileta usumbufu kwa watumiaji wa barabara hiyo kwa kufungwa na kushindwa kuendelea na shughuli zao hali iliyosababisha polisi kutumia nguvu kuwatawanya watu.
“Baada ya tukio hilo polisi na Tanroads tulikaa kikao cha dharura kilichokuwa kikielekeza utengenezwaji wa matuta ya haraka katika eneo hilo.
“Wakati tukiendelea na mazungumzo hayo wananchi walipata mwanya wa kukivamia kituo hicho na kukichoma moto.
“Sababu ya wananchi  hao kuchoma kituo hicho hakuna, na wamefanya jambo ambalo si la busara na wamesahau kuwa kituo hicho kinawasaidia watu wote wa eneo hilo,” alisema Kamanda Wambura.
Wambura alisema mbali na kuchoma kituo hicho pia wamechoma magari mamne ya watu binafsi yaliyokuwa yameegeshwa pembezoni  mwa kituo hicho.
Pia alisema wanamshikilia dereva wa Coaster aliyesababisha ajali  pamoja na gari hilo.
“Kwa sasa  tupo katika  zoezi  la kuwasaka na kuwakamata watu wote waliosababisha vurugu hizo ili sheria iweze kuchukua mkondo wake,” alisema Kamanda Wambura.
Mmoja wa mshuhuda wa tukio hilo, Moshi Sultan, alisema kuwa tukio hilo lilitokea saa 3:00 asubuhi baada ya gari kumgonga mwanafunzi huyo aliyekuwa anakwenda shule.
Alisema baada ya tukio hilo wananchi wa eneo hilo walikusanyika na kufunga barabara hali iliyosababisha polisi kuingilia kati na kuanza mvutano kati yao na hatimaye wananchi hao kuvamia kituo hicho  na kukichoma moto.
Alisema wananchi hao waliwasha moto kituoni hapo pamoja na tairi za gari na kudai kuwa  askari waliopo hawafanyi kazi kwa umakini.
“Kutokuwapo  kwa  askari wa kutosha katika kituo hicho kumechangia  wananchi  hao kuvamia kwa urahisi na kuchoma moto kituo hicho,”alisema.
Katika tukio jingine, moto mkubwa umezuka na kuteketeza nyumba yote inayomilikiwa na Hamisi Katori iliyopo katika mtaa wa Mabanda Marefu Ukonga Mombasa jijini Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Lucas Mkondya, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa chanzo cha moto huo ni hitilafu ya umeme.
Alisema wakati moto huo ukiendelea kuwaka alikuwepo mtoto mdogo mwenye umri wa miaka miwili aliyetambulika kwa jina la Mohamed Shabani ambaye alikuwa amelala ndani lakini msamaria mwema alifanikiwa kumuokoa.
Mkondya alisema moto huo uliteketeza nyumba yote, mali na thamani zilizoteketea kwa moto bado hazijafahamika.
Alisema hakuna madhara kwa binadamu, moto ulizimwa na kikosi cha Zimamoto Uokoaji cha Jiji kwa kushirikiana na wananchi wa eneo hilo.

No comments:

Post a Comment