MWENYEKITI WA CHAKUA, HASSAN MCHANJAMA (KUSHOTO), AKIWA NA OFISA WAKE, GERVAS RUTAGUZINDA |
CHAMA cha Kutetea Abiria (Chakua), kinatarajia kukutana na
Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa), ili kujadili tozo ya sh. 7000 ya kuvusha magari
ya kusafirisha abiria (daladala), katika daraja la Kigamboni ambayo ina lalamikiwa
na wamiliki wa vyombo hivyo kuwa ni kubwa.
Mwenyekiti wa Chakua, Hassan Mchanjama, aliyasema hayo
baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wa miliki wa daladala hizo, kudai kwamba
wameshindwa kulipa tozo hiyo, hivi sasa baadhi yao wamesitisha huduma kwa vile
wamekuwa wakipata hasara kila waanapovusha magari yao.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Mchanjama, alisema
lengo la kukutana na Temesa wiki ijayo ni kutaka kuona wamiliki hao
wanasikilizwa lakini kubwa ni kutetea ambiria wao.
Alisema, wamefikia hatua hiyo baada ya kusikia kuwa baadhi
ya wamiliki wa daladala hizo kusitisha huduma katika ruti hiyo, kwa kuogopa
tozo hiyo kwa kila safari, hali ambayo imesababisha kukosekana kwa usafiri kwa
wakazi wa Kigamboni.
“Chakuwa imepokea malalamiko kutoka kwa abiria pamoja na
wamiliki wa daladala kuwa daladala zao zinatozwa ushuru wa sh.7000 kwa kila
safari moja kwa siku karibu sh. 150,000 huku
wakipata hasara kutokana na hali hiyo wamiliki wameacha kupeleka magari na
kufanya abiria wahangaike kwa kukosa usafiri.
“Tunatambua juhudi za serikali ni kuwapunguzia adha ya
usafiri wananchi wake, lakini kutokana na malalamiko hayo ya abiria yanaondoa
matumaini yao ya kuondokana na adha hiyo ya usafiri kwani hivi sasa baadhi
wameanza kusafiri na vyombo vya majini ambavyo usalama wake ni mdogo hivyo
kuhatarisha maisha ya abiria hao,”alisema Mchanjama.
Mchanjama, alisema Chakua wanatarajia kuishauri Temesa
kuangalia tozo hiyo upya kwa lengo la kuifanyia marekebisho ili wamiliki hao
waweze kutoa huduma kwa abiria wao ambao hivi sasa wanataabika.
No comments:
Post a Comment