WABUNGE wanaotokea katika maeneo ya jamii ya wafugaji wamepanga kukwamisha Bajeti ya Waziri wa Malisili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe,kutokana na kauli yake ya kudai kuwa mifugo ya Tanzania haifai huku nyama yake ikiwa na sumu.
Mkakati huyo unatarajiwa kufanyika mwanzoni mwa wiki wakati
waziri huyo atakapowasilisha hotuba yake ya kuomba kupitishiwa bajeti ya wizara
hiyo ya mwaka 2016/17.
Waziri Profesa Maghembe anatarajia kusoma hotuba yake bungeni
Juni 24, mwaka huu ambayo itajadiliwa kwa siku mbili huku wabunge wanaotoka
mikoa ya wafugaji wakijiandaa kukwamisha bajeti hiyo isipite.
Walisema sababu kubwa ya kukwamisha bajeti hiyo ni kunatokana
na kauli yake ya hivi karibuni aliyoitoa kwenye kipindi maalumu kwenye moja ya
kituo cha televisheni kuwa mifugo ya Tanzania haina thamani.
Mbunge wa Nzega Mjini, Hussen Bashe (CCM) alisema, waziri
huyo amejiweka katika nafasi ngumu kutokana na kutoa kauli ambayo imewaacha
wafugaji njiapanda.
Bashe alisema, hakuna maeneo ambayo yanaweza kuwasaidia
wafugaji kwa sasa kutokana na ranchi kuhodhiwa na vigogo.
“Binafsi namheshimu
sana Profesa Maghembe, namuomba aombe radhi kwa kauli yake na akishindwa lazima
tutabanana huko ndani, kwanza alitoa hoja dhaifu sana kwamba pato la mifugo ni
dogo wakati anajua wafugaji hawajawezeshwa,” alisema.
Mbunge huyo alisema wafugaji wamehesabiwa kama wakimbizi
katika nchi yao na walibaguliwa tangu mwanzo pale Tanzania iliposema ni ya
wakulima na wafanyakazi lakini kundi la wafugaji likaachwa nyuma.
Bashe alisema, haiwezekani kupitisha bajeti ya Profesa
Maghembe kwa kuwa kauli yake ni ya kuwabeza wafugaji.
Naye Mbunge wa Monduli, Julius Kalanga (Chadema) alipinga
kauli ya Waziri Maghembe ya kuwataka wafugaji
hao kuondoka kwenye hifadhi ifikapo Juni 15 mwaka huu.
Kalanga alisema kuna shida nchini kwa kuwa hakuna sera ya
mifugo na mfumo wa utungaji kutokana na Bunge kupitisha sheria zilizotungwa na
serikali.
Naye Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mwigulu Nchemba,
aliwataka wafugaji kutokuwa na wasiwasi kwa kuwa hakuna mtu atakayeondolewa
kwenye maeneo yao hadi taratibu zingine zitakapofanyika.
Profesa Maghembe akizungumza katika kipindi hicho alisema
kuwa mifugo ya Tanzania inaliingizia taifa pato kidogo kwa hiyo haina faida
kubwa ukilinganisha na pato litokanalo na Maliasili na Utalii la wanyama.
No comments:
Post a Comment