KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Saturday 11 June 2016

MFUMUKO WA BEI WA TAIFA WAONGEZEKA MEI

OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS), imesema Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa Mei, 2016 umeongezeka kidogo hadi kufikia asilimia 5.2 kutoka asilimia 5.1 ilivyokuwa katika kipindi cha Aprili, 2016.
Hali hiyo inamaanisha kuwa kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Mei, 2016 imeongezeka kidogo ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Aprili, 2016.  Akizungumza na wa andishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk. Albina Chuwa iliyotolewa leo Jijini Dar es Salaam, kuongezeka kwa Mfumuko wa Bei wa mwezi Mei, 2016 kumechangiwa na kuongezeka kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula.
 Alisema, baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa mfumuko huo wa bei ni pamoja na asilimia ikiwa ndani ya mabano kuwa ni mahindi (1.5), unga wa muhogo (6.2), nyama ya kuku (2.6), njegere (5.8), mihogo mibichi kwa (8.0) na ndizi za kupika (2.7).
“Pia bidhaa zisizo za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa Mfumuko wa Bei ni pamoja na mafuta ya taa (2.9), mkaa (2.5), dizeli (4.6), petrol (2.5) na vifaa vya michezo (7.8).
Dk. Chuwa alifafanua kwa kusema mfumuko huo wa bei katika kipindi cha Mei, 2016 unaopimwa kwa kipimo cha mwezi umebaki kuwa asilimia 0.5 kama ilivyokuwa Aprili, 2016. Aidha, Fahirisi za Bei zimeongezeka hadi 103.00 katika kipindi cha Mei, 2016 kutoka 102.46 mwezi Aprili, 2016.
 Aidha, ulinganifu wa mfumuko wa mei kwa baadhi ya  nchi  za Jumuia ya Afrika Mashariki, inaonyesha kuwa Mfumuko wa Bei nchini Uganda kwa mwezi Mei, 2016 umeongezeka hadi kufikia  asilimia 5.4 kutoka asilimia 5.1 kwa mwezi Aprili, 2016.
 Dk. Chuwa, akisema kwa upande wa Kenya, Mfumuko wa Bei umepungua hadi kufikia asilimia  5.00 kwa mwezi  Mei, 2016 kutoka asilimia 5.27 iliyorekodiwa mwezi Aprili, 2016.
 Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa kipimo cha mwaka unapima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi.
 

No comments:

Post a Comment