KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Wednesday 25 October 2017

Kamwelwe ataka upatikanaji maji ya uhakika



NA ASHA MWAKYONDE, DODOMA

WAZIRI wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isaac Kamwelwe, ameziagiza mamlaka za maji kote nchini kuhakikisha ifikapo mwishoni mwa Juni 2018, upatikanaji wa maji safi na salama unafikia asilimia 86.
Akizungumza juzi mjini Dodoma alipokuwa akifungua kikao cha wizara hiyo na watendaji wakuu wa mamlaka za maji safi na usafi wa mazingira Tanzania Bara, Kamwelwe alisema kwamba vi vema viongozi hao wakahakikisha kuwa katika miji mikuu na midogo upatikanaji wa maji safi na salama unafikia wastani usiopungua asilimia 70 ifikapo mwishoni mwa Juni 2018.
“Kama mnavyofahamu ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2015-2020 inatuagiza tuhakikishe kuwa ifikapo mwaka 2020 upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi unafikia asilimia 95 kwa miji mikuu ya mikoa, asilimia 90 kwa miji mikuu ya wilaya, miji midogo na maeneo yanayohudumiwa na miradi ya maji ya kitaifa na asilimia 85 maeneo ya vijijini,” alisema Kamwelwe.
Aliongeza kuwa ili kufikia malengo hayo lazima kuwe na tabia ya kujipima kila mwaka ili kujua wanapiga hatua kiasi gani kufikia lengo kuu.
Aidha, alisema kuwa katika kufikia malengo hayo wanatakiwa kuhakikisha kuwa changamoto ya upotevu wa maji wakati yakisafirishwa kumfikia mlaji inapatiwa ufumbuzi.
Naye Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Juma Aweso, aliwataka wakurugenzi wa mamlaka za maji safi na usafi wa mazingira nchini kutoa ushirikiano ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa bidii ili kuweza kufikia malengo.


No comments:

Post a Comment