KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Wednesday 25 October 2017

Ugatuaji madaraka waongeza kasi ya kazi

NA HAMIDA RAMADHANI, DODOMA

IMEELEZWA kuwa dhana ya ugatuaji madaraka kwa watumishi wa umma imeleta mafanikio na mabadiliko katika utendaji kazi.
Akizungumza jana wakati akifungua mkutano wa tathmini ya maboresho ndani ya utumishi wa umma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Selemani Jafo, alisema kuwa watumishi wa sekta ya umma wanapaswa kuelewa na kusimamia dhana ya ugatuaji wa madaraka hayo na kwamba tathmini itakayofanyika ilete malengo mazuri katika utendaji kazi kwa kujitoa kuwatumikia wananchi.
“Nategemea tathmini mtakayoifanya italeta malengo mazuri katika utendaji wenu ili kuleta maendeleo kwa nchi yetu hasa kipindi hiki ambacho tunafanya jitihada za kuelekea uchumi wa kati wa viwanda,” alisema.
Mbali na hayo Jafo alisema watumishi wa umma wanapaswa kuzingatia vipaumbele vya utumishi kwa kuhakikisha kwamba wanajituma kwa bidii na kuleta mafanikio kwa wananchi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza, aliishukuru serikali kwa kufikia hatua hiyo ya ugatuaji na kwamba kwa kuzingatia vipaumbele vya utumishi watahakikisha wanatimiza malengo ya tathmini hiyo.

Mwisho

No comments:

Post a Comment