KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Sunday, 22 March 2015

ZITTO: ACT KINAKUBALIANA NA IMANI YANGU KISIASA

Zitto Kabwe akikabidhiwa rasmi kadi ya uanachama wa ACT

NA MWANDISHI WETU

MBUNGE wa zamani wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe amesema amejiunga na Chama cha ACT kwa sababu  anaamini ndicho chama  kinachoendana na yale aliyokuwa akiyapigania kwa miaka yote tangu aanze siasa, ambacho ni kuweka mbele maslahi ya Taifa.
Zitto aliyasema hayo jijini Dar es Salaam leo, wakati alipozungumza na wandishi wa habari kuhusu kung’atuka ubunge aliyoupata akiwa mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kujiunga na ACT.
“Kwa kifupi nimepigania uzalendo kwa nchi yangu na huu ndiyo msingi mama wa Chama cha ACT, kama mnavyojua mimi ni mjamaa na ninaamini kwa katika misingi ambayo Mwalimu Nyerere aliisimamia,”alisema Zitto.
Alisema alijiunga na chama hicho kwa sababu kinakubaliana na imani yake ya siasa ya ujamaa na kujitegemea, hivyo yale yote aliyokuwa akiyapigania yataweza kufanikiwa kutokana na bidii, umakini na weledi ambao utakuwa msingi bora wa maendeleo.
Aidha, chama hicho  ACT ni chama kinachoamini katika misingi ya uadilifu, kimeweka miiko na maadili ya viongozi katika kuhakikisha hayo  viongozi wote wanapaswa kukubaliana nayo ili yawaongoze katika utekelezaji wa majukumu yao.
“ACT ni chama pekee nchini kinachokubaliana na Itikadi ya Ujamaa na kinaamini katika Falsa ya Unyerere ikiwa na lengo la kurudisha nchi katika misingi ya taifa.
“Naamini kuwa miiko na maadili kwa viongozi ni mwanzo wa kuhakikisha kwamba jamii yetu inaishi katika uadilifu na kwamba viongozi  wanakuwa mfano wa uadilifu katika jamii,”alisema Zitto.
Zitto alisema kingine kilichomvutia katika chama hicho ni kwamba rasilimali za Taifa lazima zitumike kuondosha umasikini wa Watanzania.
Akijibu maswali kuhusu kudaiwa kwake kama yeye ni kibaraka wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alisema kwanza hapendi kuangalia masuala ya nyuma bali huu ni wakati wa kuangalia watayatuaje matatizo ya wananchi.
Hata hivyo Zitto, alisema siyo sasa hihi kujibu swali hilo na baadala yake wakaulizwe hao wanaosema hivyo.
“Labda ni waulize ni mbunge gani bungeni aliwahi kutoa hoja nzito, ambazo mara kadhaa zimekuwa mwiba, hoja hizo zimefanya hadi baadhi ya mawaziri kuondolewa kwenye nyadhifa zao,”alisema Zitto.
Zitto aliingia kwenye kashfa ya uhaini mwaka juzi, kashfa iliyomfanya avuliwe nyadhifa zake zote ndani ya chama hata hivyo chama kilipopanga kumjadili Zitto alikimbilia mahakamani kuzuia asijadiliwe.
Hata hivyo, wiki moja iliyopita Zitto ameshindwa kesi hiyo hali iliyomfanya Mwanasheria Mkuu wa Chadema akiwa katika ofisi za Makao Makuu ya chama hicho kwamba alitangaza kuwa Chama hicho kimemfukuza uanachama.


No comments:

Post a Comment