NA MWANDISHI WETU
WAANDISHI wa vyombo mbalimbali vya habari nchini
wamepatiwa mafunzo ya jinsi ya kuandika habari za kilimo cha ufugaji wa kuku
ambao utampatia maarifa msomaji anayetahitaji kufuga kuku kwa mara ya kwanza.
Mafunzo hayo ya siku mbili yalitolewa na Mradi
wa Mkulima Mbunifu, ambao unasimamiwa na Biovision Africa Trust, yalifanyika
mkoani Arusha mwanzoni mwa wiki hii.
Mradi wa Mkulima Mbunifu ni mradi wa
mawasiliano, ambao kwa namna moja au nyingine unaeneza na kutoa elimu ya kilimo
endelevu kwa wakulima nchini na nchi za jirani.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo juzi,
Msimamizi wa mradi huo nchini, Ayub Nnko, alisema anaamini mafunzo hayo yatawasaidia
waandishi hao, kuandika habari za ufugaji kwa usahihi bila ya kuacha maswali
kwa wadau wa kilimo.
Alisema waliamua kutoa mafunzo hayo baada ya
kubaini upungufu wa uandikwaji wa habari za kilimo cha ufugaji kama vile wa kuku, ambapo kila wakulima walipozisoma
walibaki na maswali.
“Sasa ninaamini baada ya mafunzo haya utakuwa mwanzo mzuri kwa nyie washiriki kwenda
kuandika na kuwafikishia taarifa sahihi ambazo zitawasaidia wakulima na
wafugaji na kuifanya shughuli hiyo kuwa rahisi kwao,” alisema Nnko.
Nnko aliwasihi
wananchi kuacha kukidharau kilimo, kwani maisha ya kila mwanadamu
hayawezi kuendelea bila kuhusisha kilimo ambacho kimekusanya mambo mbalimbali
ikiwemo ufugaji.
Watoa mada katika mafunzo hayo walikuwa ni John
Cheburet na Caroline Nyakundi kutoka Kenya,
ambao walisema mradi huo ambao unafadhiliwa na Biovior Fundation for Ecological, Switzerland,
unaendeshwa kwa ushirikiano wa nchi hizo mbili.
Mradi huo nchini Kenya umeanzishwa mwaka 2010 kisha mwaka 2011ukaingia
Tanzania.

No comments:
Post a Comment