![]() |
| Mkurugenzi Mkuu wa Repoa, Profesa Wangwe |
MTAFITI
Mwandamizi wa Taasisi ya Center for Development (CGD), Mujobu Moyo, amesema
Tanzania kama nchi nyingine zinazoendelea inakabiliwa na changamoto nyingi
ikiwemo rushwa na vurugu za kisiasa ambazo zinaweza kusababisha gesi iliyogunduliwa
ikashindwa kuwanufaisha wananchi wake.
Kauli
hiyo aliitoa wakati wa mkutano wa Watanzania zaidi ya 400 kutoka wilaya
mbalimbali nchini, ambao walikutana jijini Dar es Salaam jana, kujadili na
kutoa maoni kuhusu ni jinsi gani mapato yatakayotokana na gesi yatawanufaisha
wananchi wote nchini bila ya kubagua.
Mkutano
huo unatokana na kugundulika kwa hazina kubwa ya gesi nchini ambayo inategemewa
kukuza pato la taifa zaidi ya mara 15 kuliko la sasa.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini jana, Moyo alisema mkutano huo umeandaliwa na
taasisi hiyo kwa kushirikiana na taasi ya utafiti ya kuondokana na umaskini
nchini Repoa.
“Mkutano
huu utakuwa wa kwanza wa aina yake wa kuwashirikisha wananchi wa kawaida katika
utafiti unaohusiana na jinsi sera mbalimbali zinavyotungwa na kutekelezwa kwa
matakwa ya matajiri katika nchi zinazoendelea bila kuwaangalia wananchi wa
kawaida wa hali ya chini,” alisema Moyo.
Moyo
alisema ili kuepuka changamoto hizo viongozi wanapaswa kuweka usimamizi mzuri
wa mapato ambayo yatatokana na gesi hiyo, yatatoa mustakabali wa nchi katika
siku zijazo.
“Wananchi
wanapaswa kwanza kueleweshwa juu ya mchakato mzima na kushirikishwa kutoa maoni
yao ni jinsi gani mapato yatakayotokana na rasilimali hii yataleta manufaa kwa
wote ili kuepuka makosa yaliyojitokeza katika nchi nyingine kwa kosa la
kutowashirikisha wananchi katika masuala yanayohusu rasilimali za taifa,”
alisema Moyo.
Moyo
alisema utafiti huo unalenga kufuta dhana iliyozoeleka kuwa Watanzania wa
kawaida hawana haki ya kutoa mawazo katika masuala ya kitaifa kama lilivyo
suala hilo la gesi ambalo limekuwa likijadiliwa na wasomi na wanasiasa.
Mkurugenzi
Mkuu wa Repoa, Prof. Samuel Wangwe,
alisema kuongezeka ghafla kwa pato kutokana na rasilimali hizo kunaweza kuleta
athari mbalimbali kwa taifa badala ya faida kama vile kuongezeka kwa vitendo
vya rusha na kuvurugika kwa uchumi.
Athari
nyingine ni kuongezeka kwa umaskini na kupunguza kukua kwa demokrasia nchini.
Prof.
Wangwe alisema hayo yote yanajitokeza iwapo nchi inakuwa na rasilimali nyingi
na kundi la wananchi wa hali ya chini na wasio na elimu kutopewa taarifa sahihi
na za kutosha juu ya kinachoendelea.

No comments:
Post a Comment