| Makamba, akipongezana na wanachama wenzake mara baada ya kumaliza kutangaza nia. |
MBUNGE wa Bumbuli, January Makamba amesema endapo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitamteua kuwania urais na kushinda, atafumua mfumo mzima wa uongozi na atakuwa na vipaumbele vitano.
Makamba, aliyasema hayo jana wakati akitangaza nia ya kuomba ridhaa ya kuteuliwa kuwa mgombea wa urais kupitia CCM, katika sherehe iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Alivitaja vipaumbele hivyo kuwa ni kukuza kipato cha watu na kwamba msingi wa maendeleo ya nchi sio mapato ya serikali, bali ukubwa na uhakika wa kipato cha Watanzania.
Alisema kipaumbele cha pili kitakuwa kupatikana kwa huduma bora za jamii na kiuchumi na kipaumbele cha tatu ni utawala bora, wa haki na wa sheria ambao msingi wa amani ya nchi yetu ni haki.
“Wananchi wengi hawana uhakika wa kupata haki zao waendapo polisi au mahakamani, tutazijenga upya taasisi ya usimamizi wa utawala na haki za watu, zikiwemo mahakama na jeshi la polisi.
“Tutakabiliana na tatizo la ubadhirifu wa mali ya umma kwa nguvu zote na tutahakikisha ripoti ya CAG ikitolewa, viongozi ambao taasisi zao zimekutwa na makosa wanakaa pembeni siku hiyo hiyo na hatua za kisheria, za kipolisi, za kimahakama zinaanza siku inayofuatia,” alisema Makamba.
Nne ni usimamizi wa uchumi ambapo alisema Serikali yake itaimarisha uwezo wa taasisi za usimamizi wa uchumi ikiwemo Wizara ya Fedha, Tume ya Mipango, Benki Kuu na Mamlaka ya Mapato, akibainisha kuwa atazipa mamlaka na rasilimali-watu ili ziweze kudhibiti mfumuko wa bei na kuporomoka kwa thamani ya shilingi.
Pia nakisi ya bajeti, kupungua kwa hifadhi ya fedha za kigeni, kukua kwa deni la taifa na kusimamia uwekezaji wa kimkakati wa sekta binafsi.
Alisema kama ambavyo tuna Baraza la Usalama wa Taifa sasa, ataunda Baraza la Uchumi la Taifa litakalojumuisha wataalamu kutoka taasisi za umma za usimamizi wa uchumi, magwiji wa uchumi kwenye nchini, pamoja na wawakilishi wa sekta binafsi.
Kipaumbele kingine cha tano ni amani, umoja na usalama wa mali na maisha ya wananchi.
Aidha, alisema nchi yetu iko katika njia panda, Katika miaka 10 ijayo, Tanzania inaweza kuchukua njia mojawapo kati ya hizi mbili: inaweza kupiga hatua kubwa ya maendeleo na hali ya maisha ya wananchi wote kuboreka.
Makamba alisema lakini vilevile, ipo hatari ya taifa letu kupasuka kutokana na dalili za mpasuko wa kidini, mmomonyoko wa maadili kwenye jamii, kuporomoka kwa imani ya wananchi kwa dola, dalili za ufa katika Muungano, umaskini na tofauti kubwa ya kipato baina ya wananchi.
Aliongeza kuwa aina ya uongozi utakaouchaguliwaa mwaka huu ndio utaamua mustakabali wa nchi hii, hata hivyo alisema baada ya miaka 50 ya uongozi wa kizazi kilichopita, sasa ni wakati wa nchi
kuongozwa na viongozi wa aina mpya, wenye mtazamo mpya, fikra mpya, maarifa mapya na majawabu mapya.
Alisema kwa msingi huo, ataanza kwa kusema kwamba Serikali atakayounda itaendeshwa na falsafa ya uwezeshaji mpana wa wananchi – kiuchumi, kisiasa na
kijamii.
Makamba alisema hiyo itawezekana kwa kupunguza gharama za ujenzi na uwekezaji kwenye viwanda vya vifaa ya ujenzi, kama vile viwanda vya nondo, mabati, simenti, vigae na vioo.
“Tutahakikisha kwamba wakandarasi wa miradi hii ni makampuni ya ndani yatakayohifadhi na kuwekeza fedha hizo hapa ndani, lengo langu ni kuwezesha wakandarasi wa ndani kiufundi, kiutawala na kifedha na kuwawezesha kupata walau asilimia 80 ya miradi yote ya miundombinu inayojengwa kwa fedha za umma ndani ya miaka kumi ijayo.
Kuhusu elimu alisema kuwa Serikali yake itaondoa shaka na kumaliza kabisa mjadala kuhusu dira ya elimu nchini, kwamba ataongozwa na dira ya elimu inayochochea vijana kujiajiri, inayochochea udadisi, inayochochea ubunifu, inayochochea uthubutu, nidhamu, weledi na uzalendo.
Alisema itatengeneza mitaala mipya na thabiti kabisa inayokidhi mahitaji ya mazingira na changamoto za sasa na mahitaji ya uchumi wa kisasa, mahitaji ya jamii na mahitaji ya taifa kwa ujumla.
“Tutawafundisha watoto wetu kwa lugha zote mbili, ya Kiswahili na Kiingereza kwasababu ni jambo linalowezekana.
Tunasema ualimu ni wito lakini haipaswi kuwa adhabu. Tutazitatua
changamoto za walimu, ikiwemo mazingira yao ya kazi, motisha na
hamasa yao ya kufundisha ikiwemo mishahara yao, kupandishwa
madaraja, mafunzo yao ya ziada ya kujiendeleza.
Vilevile, hatutaingiza siasa kwenye maendeleo ya elimu,”alisema.
Alisema tutaweka uongozi thabiti na wa kizalendo kwenye sekta ya elimu utakaokabiliana na changamoto za uendeshaji na utawala wa sekta yaelimu, ikiwemo masuala ya ukaguzi, usimamizi wa walimu, uidhinishaji na usambazaji vitabu kwenye mashule, upelekaji na matumizi ya fedha za uendeshaji wa shule na mambo mengineyo.
Pia alisema kuwa Ili kuchukua vijana wengi wanaoishia darasa la saba na kidato cha nne, tutajenga Chuo kikubwa cha ufundi kwenye kila Wilaya ya nchi yetu kwa kushirikiana na sekta binafsi.
RUSHWA
Alisema kuwa njia ya kwanza ni kisheria, kimfumo na kitaasisi; njia ya pili ni kijamii.
Kwanza, ni kuiwezesha TAKUKURU kuwa na mamlaka kisheria yakuwashitaki watuhumiwa wa rushwa moja kwa moja mahakamani.
Pia,tuanzishe Mahakama Maalum ya Uhujumu Uchumi ambayo itahusika na makosa ya rushwa; ubadhirifu wa mali ya umma; ukwepaji kodi; kuiba, kunufaika au kutaka kuiba au kutaka kunufaika na mali ya umma; na makosa mengine ya aina hii.
Pia serikali yake itaanzishwa Kurugenzi ya Uchunguzi na Mashtaka ya Uhujumu Uchumi.
Tutaiwezesha Mahakama hii na Kurugenzi hii bila ukomo wa
kirasilimali kuifanya kazi hii vizuri.
Mwisho Makamba alimalizia kwa kusema hagombei nafasi hiyo kwa kupambana na mtu bali anagombea nafasi hiyo kwa ajili ya kupambana na matatizo ya wananchi.
No comments:
Post a Comment