KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Friday, 15 April 2016

TANZANIA YAPATA TEKNOLOJIA MPYA YA UJENZI KUTOKA CHINA



TANZANIA imefanikiwa kupata teknolojia mpya kutoka nchini China inayosaidia makandarasi wa majengo kuweza kujenga jengo la ghorofa moja kwa siku 12 badala ya siku 35 kama ilivyokuwa awali.
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, aliyasema hayo juzi wakati wa maadhimisho ya miaka 10 ya kampuni ya Group Six International (GSI) yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, ambayo pia yalihudhuriwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage.
Akizungumza jijini Dar es salaam juzi, wakati wa maadhimisho hayo, Makamu wa Rais, alisema hakuna taifa lililoendelea bila kuwa na maendeleo kwenye teknolojia jambo ambalo linasababisha kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
“Mwekezaji kama huyu ni mfano wa kuigwa, licha ya kuwekeza nchini kwetu, kaleta teknolojia mpya inayookoa muda na fedha zao na kaamua pia kuwafundisha watanzania ili nao watumie teknolojia hiyo,ni jambo la kupigiwa mfano,”alisema.
Makamu wa Rais, teknolokia hiyo itasaidia kuokoa fedha na muda ambao uliokuwa ukipotezwa na wajenzi kutokana na kutumia teknolojia za kizamani.
Akizungumzia suala la elimu, Makamu wa Rais, alisema kuwa kila mwenye uwezo wa kiuchumi anawajibu wa kuchangia maendeleo ya Tanzania na kuwa hakuna maendelo yoyote yanayoweza kupatikana kama hakuna wataalamu waliyoelimika.
Katika maadhimisho hayo Makamu wa Rais alikabidhiwa hundi ya Sh.Milioni 20 ambazo zilizotolewa na GSI kwa ajili ya kusaidia maendeleo ya elimu kwenye shule mbili zilizoko Mikocheni, jijini Dar es salaam.
Akizungumzia suala la ulipaji kodi, Mwenyekiti wa kampuni hiyo, aliyejitambulisha kwa jina la Huang alisema kuwa kampuni yake inatambuwa umuhimu wa kodi kwa hiyo wamekuwa wakilipa kodi bila kushurutishwa na kwamba kwa miaka hiyo 10 waliyowekeza hapa nchini tayari wamelipa zaidi ya shilingi bilioni 12 kama kodi pekee.
“Tumekuwa tukihakikisha tunalipa kodi stahiki kwa wakati na kwa uaminifu na bila kushurutishwa kila uwekezaji wetu tunahakikisha tunafuata sheria zote za Tanzania ili kuwa mfano kwa wawekezaji wengine hapa nchini,”alisema Huang.
Aidha, Huang, alimfahamisha Makamu wa Rais, kuwa wamedhamiria kujenga mahusiano mazuri kati yao na jamii inayozunguka miradi yao, watakuwa na michango endelevu kwenye sekta mbalimbali ili kuhakikisha Tanzania inasonga mbele kimaendeleo ili kufikia lengo la kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo 2020.
Kuhusu utamaduni, Huang alimwambia Makamu wa Rais, kuwa wamekuwa wakitumia lugha ya Kiswahili katika mawasiliano baina ya Watanzania na wachina huku pia akisifia Kiswahili kuwa kimeshika nafasi kwenye vyuo vingi vya China na kuifanya kuwa lugha inayozumzwa na raia wa China.

No comments:

Post a Comment