KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Wednesday, 25 February 2015

POLOSI LINDENI MAANDAMANO YA ALBINO



 MAKALA
BAADA ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi kuendelea kujitokeza kwa kasi ya kutisha, baadhi ya wadau hivi sasa wako katika mchakato wa kufanya maandamano ya amani.
Maandamano hayo ya amani yanatarajiwa kufanyika mwanzoni mwa Machi mwaka huu, ambayo yatakuwa ya nchi nzima na yamelenga kupinga ukatili huo na kuishinikiza serikali kuwachukulia hatua kali wote wanaohusika.
Kwani tangu kuibuka kwa mauaji hayo mwaka 2006, hadi hivi karibuni alipouawa mtoto Yohana Bahati, albino 76 wamekwisha kuuawa kikatili na watu wasiojulikana.
Mauaji hayo yanailetea nchi aibu katika jumuia ya kimataifa na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa uchawi.
Vitendo hivyo vya mauaji ya albino kwa kiasi kikubwa vinahusishwa na imani za kishirikina.
Matokeo ya vitendo hivyo, kuendelea kutokea huku kukiwa hakuna ufumbuzi wa kukomesha ukatili huo umefanya hadi mashirika ya Umoja wa Mataifa kuingingilia kati.
Shirika ambalo limejitokeza na kupaza sauti ni lile la Maendeleo (UNDP),  ambapo limetaka serikali kukomesha mashambulio hayo.
Kutokana na tatizo hili kuzidi kuwa sugu wadau hao sasa wameanza mchakato wa maandalizi ya maandamano ya amani ili kuweza kupeleka kilio chao kwa rais aweze kushauriana nao kwa ajili ya kupata suluhu ya kudumu itakayomaliza tatizo hili.
Katika maandamano hayo pia kutafanyika sala maalumu kwa ajili ya  wote waliopoteza maisha yao kwa kuuawa kikatili.
Katika hili ni vema kila mmoja wetu ambaye anaheshimu haki za binadamu akajitokeza kuwaunga mkono ndugu zetu katika kupinga mashambulizi dhidi yao.
Sitarajii kama kutakuwa na pingamizi lolote kuhusu maandamano hayo, ambayo yana ujumbe muhimu.
Nasema hivyo, kwa vile kuna tabia ya Jeshi la Polisi kupenda kuingilia kati kila yanapotaka kufanyika maandamano tena bila kuangalia kinachopiganiwa na makundi husika.
Mbaya zaidi jeshi hilo limekuwa likiyapiga marufuku maandamano siku moja kabla, huku wahusika wakiwa wameshapeleka barua ya kuomba kibali mapema.

Kwa vile tukio la maandamano ya albino ni tofauti na mengine, huku wakiwa tayari zaidi ya wiki moja wamekwisha kutoa taarifa, sidhani kama itakuwa ni busara kwa polisi kusubiri hadi ibakie siku moja ndipo watangaze kuyasimamisha.
Cha msingi ni jeshi hilo kujiandaa katika kuwapa ulinzi wa kutosha wadau hao ili waweze kufikisha ujumbe wao kwa wanaohusika.
Pia niwatahadhalishe baadhi ya watu ambao mara nyingi hupenda kuvamia makundi ya maandamano kwa lengo la kuanzisha vurugu ambazo zitawafanya wapate nafasi ya kufanya uhalifu.
Kwani kama wapo watakaojitokeza kwa nia hiyo watambue wadau hao wamejipanga kuwaumbua kabla ya polisi hawajawashughulikia.

Huu si wakati wa kuyafanyia dhihaka maandamano haya, kwani yana lengo la kupigania haki ya utu wa mwanadamu ambao wanaishi kwa mashaka makubwa katika nchi yao.

No comments:

Post a Comment