KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Wednesday, 11 March 2015

DK. MWELE
TAASISI ya taifa inayojihusisha na Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), imesema vyombo vidogo vya plastiki na matairi ya magari vinachangia kwa kiasi kikubwa kuzalisha mbu waitwao ‘Aedes aegypti’ wanaoambukiza ugonjwa wa dengue.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Mwele Malecela, wakati akitoa matokeo ya utafiti wa ugonjwa huo, uliofanywa na taasisi hiyo mwaka jana.
Dk. Malecela alisema utafiti huo umebainisha kwa mara ya kwanza mbu wanaoambukiza virusi vya dengue katika Jiji la Dar es Salaam, kuwa ni ‘Aedes Aegypti’ na kwamba asilimia kubwa ya mbu huyo huzaliana kwenye vyombo vya plastiki na matairi ya magari.

Alisema kati ya nyumba 796 zilizokaguliwa kuwepo kwa mazalia ya mbu asilimia 38.3, zilikuwa na vyombo vya plastiki vyenye maji yanayoruhusu kuzaliana kwa mbu katika mazingira yake na asilimia 27.5 zilikutwa na vyombo vyenye viluwiluwi au mabuu ya mbu wa jamii ya Aedes.

Alisema uwiano wa idadi ya vyombo vyenye mazalia ya Aedes kwa idadi ya nyumba zote zilizokaguliwa ulikuwa ni asilimia kwenye mabano (18) Ilala, (35.3) Kinondoni na  (25.5) Temeke, huku Kivukoni ikiongoza kuwa na nyumba nyingi zilizokuwa na vyombo vingi vya plastiki vilivyokuwa vikiruhusu mazalia ya mbu.

Aliongeza kuwa uwiano wa vyombo vyenye viluwiluwi kwa vyombo vyote vilivyokaguliwa ulikuwa ni asilimia katika mabano (77.4) Ilala, (65.2), Kinondoni na (80.2) Temeke. 
Alisema viluwiluwi kutoka mazalia hayo, vilitunzwa hadi kuanguliwa 5,250 na kuwa mbu wapevu, kati yao asilimia 61.9 ya mbu walikuwa ni wajamii ya Aedes aegypti na uchunguzi wa vinasaba katika mbu hao, ulibainisha kuwa asilimia 10.3 ya mbu wa Ilala, asilimia 8.5 Temeke na 6.5 Kinondoni walikuwa na virusi vya dengue.

Dk. Malecela alisema jumla ya wagonjwa 483 walishiriki katika utafiti huo, Wilaya ya Kinondoni ndiyo iliyokuwa na wagonjwa wengi wenye homa asilimia 37.3 au maambukizi ya  virusi vya dengue asilimia 48.5.

Alisema  kati yao asilimia 37 ya wagonjwa wote walikuwa na umri wa miaka 15 hadi 29, na kati ya wagonjwa 110 asilimia 22.8 walikuwa na maambukizi ya dengue.
Aliongeza kuwa asilimia 20.9 ya wagonjwa walikuwa na maambukizi mapya na 1.9 yalikuwa maambukizi ya zamani. 

Dk Malecela alisema kundi la watu wazima wenye umri kati ya miaka 15 na 44 lilikuwa katika hatari ya maambukizi mara tatu zaidi ya makundi mengine.


Dk.Malecela alisema kutokana na matokeo hayo ni vema ufuatiliaji wa ongezeko la mbu katika jiji ukaanzishwa au kuimarishwa ili kuweza kutabiri uwezekano wa  mlipuko wa dengue katika siku zijazo, huku akitaja  gharama zilizotumika katika utafiti huo kuwa ni sh. mil. 109.

No comments:

Post a Comment