KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Sunday, 1 March 2015

KEPTEN KOMBA ALILIWA



VIONGOZI mbalimbali wa kitaifa na wabunge, wamesema kifo cha mbunge wa Mbinga Magharibi, Kepteni John Komba ni pigo kwa Taifa hususan kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Komba alifariki dunia juzi katika hospitali ya TMJ, alipopelekwa baada ya kuzidiwa ghafla akiwa nyumbani kwake Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam.
Wakizungumza na waandishi wa habari jana nyumbani kwa marehemu, viongozi hao walisema hakuna aliyetarajia kifo hicho, lakini hakuna wa kumlaumu kwani ni kazi wa Mungu.
Membe
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernad Membe, alisema msiba wa Komba si wa Watanzania, bali umegusa ukanda mzima wa Afrika Mashariki.
Membe ambaye pia ni Mbunge wa Mtama, alisema licha ya kuwa nembo ya upendo na ushirikiano katika chama, lakini pia alikuwa akishirika hata katika masuala ya kimataifa, kwani alikuwa akitafuta ufumbuzi wa mgogoro wa kugombea mpaka katika Ziwa Nyasa, uliyojitokeza kati ya Tanzania na Malawi.
“Kepteni Komba ametoweka haraka kama mshumaa, kwa kweli hili ni pigo ambalo halitaweza kusahaulika mara moja kwetu sisi Watanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla,”alisema Membe.
Makinda
Spika wa Bunge, Anna Makinda, alisema Komba alikuwa mcheshi na muwazi, pindi anapokuwa na jambo analisema hadharani bila hofu yoyote na ndio maana alipendwa na wabunge wenzake pamoja na wananchi.
Makinda ambaye pia ni Mbunge wa Njombe Kusini, alisema kifo hicho kimekuwa cha ghafla kutokana na kutokujua kama alikuwa anaumwa ugonjwa wowote hadi pale umauti ulipomkuta.
“Nimemfahamu muda mrefu sana, kabla hajawa mbunge, pia mimi ndiye niliyemshauri agombee ubunge nilipokuwa mkuu wa mkoa, hivyo ni pigo na simanzi kubwa ndani ya chama,” alisema.
Alisema kutokana na Kapteni Komba kufariki dunia katika kipindi muhimu ambacho chama kilikuwa kikimuhitaji, na kuomba Mungu awajaalia mtu mwingine atakayeziba pengo lake.
Dk. Slaa
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbrod Slaa, amesema kifo cha Komba kimekuwa pigo kubwa kwa taifa, kwani hakuna asiyemjua kutokana na kazi zake.
“Tunapokuja duniani hatuombi wala hatupigi hodi, pia tunapondoka ni hivyo hivyo hatuwezi kulaumu kazi ya Mwenyezi Mungu, kwani ameshaamua.
“Nafarijika kwamba ameondoka akiwa sahihi, kwani amejiandaa vizuri nikiwa na mana kiroho, hivyo Mwenyezi Mungu atampokea vema anapokwenda,”alisema.
Mwigulu
Naibu Waziri wa Fedha,  Mwigulu Nchemba, alisema kifo cha Kepteni Komba hataweza kukisahau kwa vile alikuwa mtu aliyewahi kumsaidia katika kupata ushindi kwenye jimbo lake.
Nchemba ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Mashariki,  alisema nyimbo zake alizoimba wakati wa kampeni ziliweza kuwavuta kwa wingi na kusikiliza sera za chama chao hatimaye kupigia kura za ushindi.
“Kaptein Komba alitengeneza nembo ya chama chetu, kwa kweli ameondoka katika kipindi muhimu ambacho tulikuwa tukimtegemea,”alisema Nchemba.

Nasari
Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nasari, alisema msiba huo  umemshitua, kwani alikuwa hajui kama Komba alikuwa anaumwa.
Alisema hivi karibuni Kamati ya Maendeleo na Jamii ambayo wako pamoja ilikuwa ifanye ziara nchini Ethiopia, hivyo kutokana na msiba huo ziara hiyo imeahirishwa.
Nape
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema baba yake mzazi (Mzee Nnauye) alishawishi Komba kujiunga na CCM kutoka na ushawishi  alikokuwa nao.
“Kifo hiki kimefanya ziara ya Katibu Mkuu wa CCM iahirishwe  hadi Jumatano ijayo,” alisema.
Ngeleja
Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, alisema taifa limepoteza mpiganaji wa kweli, kwani Komba alikuwa kiongozi mwenye msimamo katika yale aliyoyaamini.
“Nafikiri huu ni wakati wa msiba haipendezi kwa baadhi ya watu kufanya mzaha katika mitandao  ya kijamii kwani si ustaarabu wa Watanzania, kwani sisi sote tutapita njia hii,” alisema Ngeleja.
Migiro
Waziri wa Katiba na Sheria, Asha-Rose Migiro, alisema kifo hicho ni pigo ndani ya CCM, kwani Komba alikuwa na mchango mkubwa.
“Marehemu aliunganisha taifa kupitia nyimbo zake mbalimbali, hasa katika kipindi cha msiba wa Mwalimu Julius Nyerere, pia alikuwa na moyo wa kujituma,”aisema.
Ratiba ya mazishi
Mwili wa marehemu ulifikishwa nyumbani kwake jana jioni na leo  kuanzia saa 2 asubuhi ndugu na jamaa watapata fursa ya kuuaga.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, saa nne asubuhi, mwili wa marehemu utapelekwa katika viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam kwa ajili ya kuagwa na viongozi wa kitaifa na wananchi.
Baadaye mwili huo utapelekwa uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) majira ya saa 9:30 kwa ajili ya kusafirishwa kuelekea mkoani Ruvuma kwa mazishi yatayofanyika kesho kijijni kwake Lituhi, mkoani Ruvuma.  
mwisho

No comments:

Post a Comment