KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Tuesday, 24 March 2015

MFUMO WA BVR, HAUPASWI KUHARAKISHWA


ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba (pichani), amesema uandikishaji wananchi katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa kutumia mfumo wa Biometric Voter Registration (BVR), haupaswi kuharakishwa, kwani baada ya kazi hiyo, ni lazima Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), ifanye uhakiki wa majina ya wapigakura.
Akizungumza katika kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na Independent Television (ITV), alisema kwa uzoefu wake alipokuwa kiongozi wa timu ya waangalizi wa uchaguzi wa Jumuiya ya Madola nchini Malawi miaka 11 iliyopita, alibaini kuwa mfumo huo unaweza kuandikisha mtu mmoja mara mbili hadi nne.

“Tulikuta wanatumia BVR, utaratibu huu ni mzuri kwa kuzuia udanganyifu. Nchi ya Malawi ina takriban watu milioni tisa. Lakini tulikuta watu milioni sita wamejiandikisha. Tunaona haiwezekani zaidi ya theluthi mbili wajiandikishe kwenye uchaguzi,” alibainisha.
Aliongeza: “Tulibaini wengi walijiandikisha mara mbili tatu, nne, utaratibu huu ukijiandikisha majina mawili unafuta unabakiza moja, na hiyo ni muhimu tume ikishaandikisha lazima ihakiki, isipohakiki lazima yatafutwa, mtu atakuja kwenye kituo jina lake halipo na la mwingine lipo mara mbili na kulalamika.” 
Alisema baada ya uandikishaji kumalizika ni lazima Nec ihakiki majina hayo kabla ya kuanza kutumika kwa daftari hilo.
Jaji Warioba (pichani) alirejelea kauli yake kuwa kura ya maoni haiwezekani kufanyika Aprili 30, mwaka huu, kama ambavyo serikali imeeleza kutokana na sababu mbalimbali.
Alizitaja sababu hizo kuwa ni Nec kuandikisha wapigakura, ambao pia watapiga kura katika Uchaguzi Mkuu, huku sheria ikiruhusu kuandikisha vijana, ambao hawajafikisha miaka 18, ambao Oktoba, mwaka huu, watakuwa wamefikisha umri huo.
“Kama tunaandikisha kwa kura ya maoni, haiwezekani kwa kuwa vijana hawa watakuwa hawajafikisha umri wa kupiga kura,” alisema.
Aliongeza: “Ukiwaacha suala la tume ihakiki, lakini fedha hatuna, muda hautoshi kwa matatizo yote haya inaonekana hakuna haraka ya kukimbiza mchakato huu.”
KURA YA MAONI
Alisema ni mara ya kwanza Tanzania inakuwa na utaratibu wa kura ya maoni, na kwamba maandalizi yanahitajika sana kwa kila kitu kinachohusiana nayo.
Jaji Warioba alisema kura ya maoni ina sheria yake, ambayo imepata matatizo katika utekelezaji, ilitugwa kwa kuamini kwamba, mchakato wa mabadiliko ya katiba utakwenda kama ilivyopangwa.
Alisema sheria inasema Bunge Maalumu likimaliza kazi yake, Rais akakabidhiwa, muda wa wiki mbili atangaza katika Gazeti la Serikali, baada ya hapo ndani ya wiki moja Nec itayarishe swali, ambalo wananchi wataulizwa.
Jaji Warioba alisema baada ya hapo kwa muda wa wiki mbili, Nec itatangaza muda, ambao elimu kwa umma itatolewa, ambayo ni sawa na wiki tano na kwamba, yote yangewezekana kama kungekuwa na daftari la wapigakura.
Alisema bahati mbaya tume haikuwa imeandaa shughuli zote zikasimama hadi uandikishaji ukamilike na hadi sasa inaonekana ni vigumu kukamilisha uandikishaji kwa muda wa wiki mbili.
“Huwezi kupanga kupiga kura kama huna wapigakura, Nec ilikuwa haijaandaa wapiga kura, shughuli zote zilisimama hadi uandikishaji ukamilike,” alisema:
Aliongeza: “Nia ya kupitisha Katiba mpya mapema ni iweze kutumika katika Uchaguzi Mkuu, hiyo haiwezekani sasa, hata tukiipitisha Aprili haiwezi kutumika katika uchaguzi inahitaji maandalizi ya kutosha.”
Mathalani, alisema Katiba inayopendekezwa ina sehemu ya Nec kuundwa upya, na iwapo Katiba ingepitishwa ingelazimu kuundwa upya kwa Nec, jambo ambalo haliwezekani kwa kuwa Bunge la mwisho litakuwa limeshakaa, na hakuna uwezekano wa kubadili lolote kuhusiana uchaguzi wa mwaka huu.
“Uharaka haupo, haiwezekani… kwa sababu hiyo ni vizuri tusiharakishwe tusije kufanya makosa,” alisema.
Jaji Warioba alisema ni busara rais alipokutana na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), na kusema kura ya maoni hadi mwakani na kwamba kwa maandalizi yaliyopo inawezekana kusubiri kura hiyo kufanyika mwakani kwa kuwa ni matatizo ya kawaida kwa kuwa hakukua na daftari na haiwezekani kuandaa kura bila kuwa na daftari.
Alisema haoni madhara yoyote kwa kura hiyo kufanyika mwakani kwa kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba imemaliza kazi yake, Bunge Maalum lilifanya kazi yake, iliyobaki ni kura ambayo inaweza kusogezwa mbele kwa kuwa sheria haikutaja tarehe.
ELIMU KWA UMMA
Jaji Warioba alisema Sheri inasema Tume ya uchaguzi ndiyo itatoa elimu kwa umma juu ya Katiba inayopendekezwa na utaratibu wa kupiga kura ikiwamo kualika taasisi nyingine kushiriki kutoa elimu kwa umma.
“Ni vizuri watu wakajua Katiba inayopendekezwa ikoje na masharti yaliyopo kwenye sheria ya mabadiliko, mfano inasema Kampeni itafanywa na kamati za kampeni, hadi sasa haijaelezwa 
zitaundwa vipi, zitasajiliwa Nec, masharti yake, ili watu wajue nani wanaweza kuunda kamati, utaratibu wenyewe pamoja na uamuzi,” alisema.
THELUTHI MBILI 
Alisema sheria inasema katiba inayoenda kukubalika lazima ipitishwe kwa wingi wa kura bara na Zanzibar, kwa Zanzibar ni wazanzibari walio Zanzibar ambao wamendikishwa katika daftari la wapiga kura la serikali ya Zanzibar pamoja na wengine waliopo bara watahesabiwa kama wanzanzibar.
“Lazima waelimishwe na utaratibu ufanywe kama mtu (mnzanzibar) yupo Ngara, atapigaje kura ili aende kuhesabiwa Zanzibar, vinginevyo kutakuwa na malalamiko,” alisisitiza na kuongeza:
“Katika chaguzi zilizopita kuna watu wametoka bara wameenda Zanzibar kupiga kura, hapa malalamiko yatakuwa mengi zaidi inataka maandalizi ya uhakika.”
WATANZANIA WANAOISHI NJE
Alisema tume haina utaratibu wa kuandikisha Watanzania walio nje na kwamba ili waruhusiwe kupiga kura kinachotakiwa kutawala ni busara na kuweka utaratibu wa kuruhusu kama nchi ya Msumbiji.
“Sina matatizo kama watanzania walio nje watapata nafasi ya kupiga kura,” alisisitiza huku akisema kilichofanywa na Bunge Maalum kupitisha katiba inayopendekezwa kwa walio nje kupiga kura hawezi kuzungumzia.
AMFAGILIA MAREHEMU DK. MVUNGI
Jaji Warioba alisema aliyekuwa mjumbe wa Tume hiyo, Marehemu Senkondo Mvungi, alikuwa mmoja waliojitolea kwa kila njia, na kwmaba licha ya kuwa mwanasiasa, msomi na aliwahi kugombea Urais, wakati wa kukusanya maoni alisikiliza wenzake na hakuwa na mawazo yake pekee.
“Kwenye Tume alitusaidia sana kwa uwezo wake na alikuwa mwepesi kujitolea kufanya kazi ya zaida, alikuwa committed kutaka Katiba mpya, huko nyuma alifanya harakati zake na alianza kuandika Katiba yake, aliingia katika hili kwa moyo safi, akatumia juhudi zake na nguvu zake zote kjwa uadilifu,” alisisitiza.
Aliongeza: “Ukiona taarifa zetu tunasema tulifanya utafiti, wenyewe, wafanyakazi na tuliomba watu wafanye utafiti, mmoja wa watu waliofanya utafiti mkubwa ni Dk. Mvungi, hasa kwa mambo yanayohusu wananchi, alifanya na kutayarisha maoni.”
SHERIA YA MAADILI HAINA MENO
Jaji Warioba alisema kuna sheria ya maadili lakini haina nguvu, kwa sababu wanaosimamia ni wale wale na kwmaba ndiyo maana wananchi wametaka Azimio la Arusha lirudishwe ambalo lilishughulikia mfano kiongozi asiwe na nyumba ya kupangisha na akiwa nayo moja kwa moja bila kusubiri Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza.
“Mfano nchi ya Philipine walikuwa na sheria, wakaona ukiweka hayo mambo kwenye sheria haitakuwa na nguvu inahusu wale wale wanaoisimamia, wakaweka kwenye Katiba, nchi nyingi Afrika kusini, Namibia zimefanya hivyo na kufanikiwa,” alisema.
SAKATA LA ESCROW
Jaji Warioba alisema ukiangalia suala la maadili kwa watumishi wa umma katika sakata la akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) hakuna aliye msafi.
“Tunakwenda kwenye kipindi cha uchaguzi viongozi watakuwa na fedha nyingi sana. Wakati wa sakata la Escrow ilikuwa vigumu kujua serikali iko wapi na wabunge wako wapi, madaraka kati ya serikali na bunge huyaoni,” alisema. 

Aliongeza: “Sisi tulisema yatenganishwe, serikali iwe kando na bunge liwe kando, ili serikali isiingilie Bunge na Bunge lisiingilie serikali, sasa unakuta wanaingiliana, inakuwaje Bunge linasikiliza Katibu Mkuu, kama Bunge haliridhiki na mwendeno wa serikali linasema voter of no comfidence na haliwezi kumfukuza mtumishi wa serikali, hii ni kuchanganya madaraka, hilo nalo wamelikataa.”
PINDA AZINDUA UANDIKISHAJI
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, jana alizindua uboreshaji wa daftari hilo kwa kutumia BVR na kuwataka viongozi wa siasa wawahimize wanachama wao kujitokeza kwa wingi bila kujali tofauti za kiitikadi.
Alitoa wito huo jana katika uzinduzi huo uliofanyika kwenye Kata ya Lumumba, Halmashauri ya Mji wa Makambako, mkoani Njombe.
“Ninawasihi viongozi wa siasa tuwahimize wanachama wetu waende kujiandikisha kwa wingi. Tuache kauli za kukatisha tamaa, tuache kauli za kejeli sababu zoezi hili ni jema na lina nia ya kuwawezesha Watanzania wote kutumia haki yao ya kupiga kura,” alisema. 
Pinda alitumia fursa hiyo kuwaomba Watanzania wenye vitambulisho vya uchaguzi vya zamani na wale wasio na vitambulisho wajitokeze kwa wingi kushiriki zoezi hilo.
“Wale waliokwishafikisha miaka 18, na wale ambao watatimiza miaka 18 ifikapo Oktoba, mwaka huu wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwa sababu wasipofanya hivyo hawataweza kupiga kura kama hawatajiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,” alisema.
Mapema, akitoa taarifa kabla ya kumkaribisha Pinda kufanya uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva, alisema ana imani wadau mbalimbali wataendelea kuhamasisha wananchi washiriki zoezi la uboreshaji daftari hilo.
Akitoa ufafanuzi kuhusu mfumo wa uandikishaji wa BVR, Jaji Lubuva alisema mfumo huo siyo sawa na mfumo wa upigaji kura wa kielektroniki (e-voting) kama ambavyo wengi wanadai bali mfumo huo unafanya kazi kwa kutumia alama muhimu za mpigakura.
“Mfumo huu unatumia alama zaidi kwanza ikiwa ni picha na zaidi ni macho ya mhusika, pili ni alama za vidole na tatu ni saini ya mhusika. Mfumo huu unaweza pia kuchukua alama za mtu mwenye ulemavu wa kuona ama ulemavu wa mikono,” alisema.
Alisema uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura ni hatua ya kisheria na kwamba Tume itajitahidi kuhakikisha inafuata hatua zote wakati wa zoezi hilo.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment