NA MWANDISHI WETU
MKOA wa Kigoma ni hazina kubwa ya vipaji hapa nchini
Tanzania.
Tangu zamani kulishuhudiwa vipaji vingi toka mkoani humo hasa vya wanamichezo
na wasanii.
Mfano kwa upande wa
kandanda tutaona kwamba mkoa huo ulitingisha kwa vipaji vya wanasoka.
Kina Manara, Kitwana Manara, Sunday Manara, Kassim Manara na ndugu
zao wengine wanatoka Kigoma. Baadaye kikafuatia kizazi cha kina Edbily Lunyamilla,
Nteze John, Omari Mavumbi, Itutu Kigi na wengineo wengi.
Kwa upande wa wasanii wa muziki Kigoma imetoa watu wengi wenye
majina makubwa katika sanaa hiyo, kama Shem Karenga, Hassan Rehan
Bitchuka, Marijani Rajabu, Zahir Ally Zorro, Banana Zorro, Wema Abdallah, Nyota
Waziri na wengineo wengi.
Kwa upande wa muziki wa kizazi kipya Kigoma imetoa vijana wengi wa
muziki huo wakiongozwa na mtaalamu wa muziki, kwa maana ya kutunga, kuimba,
kucheza kila ala ya muziki na kutengeneza muziki, Emmanuel Bizimana Ntavyo
‘Bizman’. Wapo wengine kama Ally Kiba, Banana Zorro, Jacqueline Ntuyabaliwe
‘K-Lynn’ na wengineo.
Lakini pamoja na wote hao makala hii ni mahususi kwa moja ya
vipaji hivyo vya mkoa wa Kigoma ikiwa imemlenga chiriku wa muziki wa kizazi
kipya kwa sasa hapa nchini, Nassibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.
Diamond kadhihirisha kipaji cha sanaa ya muziki kutokana na
mafanikio aliyoyapata kwa muda mfupi alioutumia katika sanaa. Hiyo ni tofauti
na kipindi alichokitumia mfalme wa muzuki wa POP duniani, Michael Jackson, kuwa
kileleni mwa mafanikio kwa zaidi ya miaka 10 kati ya 1967 – 1979.
Lakini ndani ya miaka mitatu Diamond ameweza kuibeba Tanzania na
kuiweka kwenye chati ya kimataifa kwenye fani hiyo ya muziki wa kizazi kipya.
Na ninaposema ngazi ya
kimataifa sina maana ya kuvuka tu mipaka ya nchi na kuingia nchi za jirani kama
Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Zambia, Malawi, Msumbiji wala Kongo, kama
ambavyo wameweza kufanya wasanii wengine wa muziki huo wa hapa nchini,
ninamaanisha kimataifa kwa maana halisi.
Nalenga nchi za mbali na
Tanzania.
Muziki wa Diamond kwa sasa unapigwa kwenye nchi mbalimbali za
Afrika, ukiondoa nchi za Kiarabu kwa upande wa Afrika Kaskazini, ambako sina
uhakika kama muziki wa kizazi kipya una mashabiki kulingana na utamaduni wa
huko.
Kwa maana hiyo Diamond kaiweka Tanzania kwenye chati ya kimataifa
kwa maana halisi kimuziki.
Kwa sasa msanii huyo
anakula sahani moja na wasanii wa kimataifa kama kina Peter Okoye na Paul
Okoye, Wanigeria wanaounda kikundi cha P Square, ambao mara kadhaa wamemuomba
watoe naye vibao vya pamoja.
Pia yuko kwenye kiwango cha wanamuziki kama Youssou N’Ndour wa
Senegal na wengine wa aina hiyo.
Kwa eneo hili la Afrika Mashariki, nashindwa kumtofautisha Diamond
na Joseph Mayanja ‘Chameleone’. Kwa sasa wanamuziki hao wanafanana.
Tanzania iliwahi kuvuma sana duniani miaka ya nyuma kupitia kwa
wanamichezo, hususan wanariadha, kina Filbert Bayi, aliyewahi kuwa bingwa wa
mbio za mita 1500 duniani, ambaye mpaka sasa anashikilia rekodi ya mbio hizo
kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola aliyoiweka mjini Christchurch nchini New
Zealand mwaka 1974.
Wengine ni Seleman Nyambui, Adventina Mtakyawa, Juma Ikangaa,
Gidmas Shahanga na wengine wengi.
Lakini kutokana na umri kuwatupa mkono nyota hao, jina la
Tanzania limefifia katika tasinia ya michezo na kuifanya nchi yetu isahaulike
kabisa kana kwamba haipo kwenye nyanja ya michezo na burudani!
Hivyo Diamond ni kijana aliyedhamiria kulipandisha tena jina la
nchi yake kupitia tasnia ya burudani. Na niseme kwa uhakika kabisa kwamba
ameweza.
Hilo linashadidiwa na tuzo mbalimbali za kimataifa anazozipata kwa
sasa kwa upande huo wa burudani baada ya kushindanishwa na wasanii wengine wa
kimataifa toka nchi mbalimbali.
Kitu cha kipekee nilichokigundua kwa Diamond na kuhisi kwamba
pengine ndicho kinachochochea mafanikio yake ni tabia yake ya kusikiliza
ushauri na kuufanyia kazi.
Wakati fulani nilimpa changamoto, ambayo vilevile niliwahi kuitoa
kwa Chameleone nilipokutana naye Jijini Mwanza, Mei mwaka jana, kwamba kwa
kiwango alichopo hapaswi kuendelea kuimba muziki kwa kutumia mtindo wa “Play
back”, kwamba anatakiwa kuwa na vyombo vyake na kupiga muziki live.
Diamond kanielewa na kusema kwamba hilo analifanyia kazi kwa bidii
kubwa.
Kingine ni namna anavyoendesha mahusiano na jamii aliyomo. Kawaida
kuna dhana ya kwamba wasanii ni watu wasioeleweka vizuri ndani ya jamii, wahuni
na huo kuwa mwanzo wa neno usanii, kwamba fulani kanifanyia usanii ikiwa na
maana ya kanifanyia uhuni.
Lakini hilo ni tofauti kwa Diamond. Yeye anapenda kuwasaidia
wenye mahitaji kulingana na hali halisi ilivyo. Kipindi fulani kwa mfano, kwa
kuuthamini mchango wa Baba wa Muziki hapa nchini, Marehemu Muhidini Maalim
Gurumo, aliamua kumpatia gari jipya.
Huo ni usanii kwa upande wa pili anaouonyesha Diamond tofauti na
upande uliozoeleka kwa jamii.
Diamond anasema kwamba amejipangia kila mwezi kuwa anatembelea
vituo vya watoto yatima na kutoa misaada mbalimbali kadri inavyowezekana. Huo
ni mchango mwingine katika jamii anaoufanya kijana huyo.
Anawashauri vijana wenzake, hasa wasanii, wanaojiingiza kwenye
ulevi uliopindukia pamoja na matumizi ya dawa za kulevya waache mambo hayo mara
moja.
Anasema kwamba yanaharibu
vipaji na wakati mwingine kupoteza maisha. Anasema ili kulinda kipaji chake
yeye anahakikisha anaepukana na mambo hayo yasiyo na maana na yaliyo hatari kwa
maisha ya binadamu.
Diamond anasema kwamba alizaliwa Septemba 22, 1990, Kigoma.
Anasema kwamba kilichomfanya aingie kwenye muziki ni kipaji chake
kilichojitokeza tangu akiwa shule ya msingi. alikuwa akiimba kwenye kwaya ya
shule na burudani nyingine za shuleni.
Huyo ndiye Diamond Platnumz, ambaye wasanii wengine vijana
wanapaswa wamtumie kama kipimo ya mafanikio katika muziki wa kizazi kipya
wanaoufanya.
Bila shaka watakaofuata mwenendo wake watafanikiwa kama yeye
alivyo.

No comments:
Post a Comment