NA MWANDISHI WETU
HATIMAYE muswada binafsi wa kuanzishwa Baraza la Vijana la
Taifa uliyowasilishwa bungeni Oktoba 31, 2013 na Mbunge wa Ubungo John,
umepangwa kusomwa kwa mara ya pili na kujadiliwa Machi 31 mwaka huu katika
Mkutano wa 19 wa Bunge linaloendelea mkoani Dododoma.
Mnyika, alisema Muswada huo ulisomwa kwa mara ya kwanza
katika Mkutano wa 14 wa Bunge Disemba 21, 2013, umetokana maoni ya wadau
yalikusanywa Oktoba 2014 na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii.
Akizungumza na wandishi wa habari leo, Mnyika, alisema kuwa
lengo la Baraza hilo la Vijana nchini, pamoja na malengo mengine pia litawezesha
vijana kuanzia kwenye vijiji, mitaa hadi taifa kuweza kuwa na vyombo vya
kuwaunganisha vijana wa kike na wa kiume kwa ajili ya maendeleo yao na ya
taifa.
Alisema Kujadiliwa kwa muswada huo ni hatua ya pekee katika
historia ya harakati za vijana nchini kwa kuzingatia kuwa Sera ya zamani ya
maendeleo ya vijana ya mwaka 1996 ilitamka kwamba kutaanzishwa Baraza la Vijana
na suala hilo
kurudiwa katika Sera mpya ya mwaka 2007.
“Natambua mchango wa vijana na
taasisi zote za vijana mlioshiriki katika maandalizi ya muswada huu, unaitwa
binafsi kwa sababu tu ndio neno linalopaswa kutumika kwa mujibu wa Kanuni za
Bunge lakini ukweli ni kwamba huu ni muswada wenu; mimi ni mwakilishi,”alisema
Mnyika.
Hata hivyo, alisema kuwa Serikali
imekuwa ikikwepa kuhakikisha kwamba matakwa hayo ya sera tajwa yanatekelezwa
kwa wakati pamoja na kuwa suala hilo
linahusu mustakabali wa maendeleo ya vijana nchini.
Aidha, Baraza hilo
litafuatilia pia kwa karibu utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya vijana ikiwemo
kuhusu ajira, elimu na sekta zingine katika Halmashauri, Serikali kuu, katika
vyombo mbalimbali vya maendeleo na wadau wa maendeleo.
Mnyika, alisema pia Muswada huo utawezeshwa kuanzishwa kwa
Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na kulipa jukumu Baraza la Vijana kufuatilia kwa
karibu utendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana; kuhakikisha kwamba fedha
zinatengwa za kutosha na kufika kwa walengwa kuwawezesha vijana kujiajiri,
kukuza vipaji vyao na kushughulikia maendeleo yao kwa ujumla.

No comments:
Post a Comment