KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Wednesday, 25 March 2015

MWENDA: WAKAZI WA MABONDENI HAMENI

Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuph Mwenda akitoa maelekezo kwa watendaji wa Manispaa hiyo kuhusu kutafuta ufumbuzi wa chemba ya majitaka iliyofurika katika Mtaa wa Balozi Msolomi wakati wa ziara yake. Kulia kwake ni Naibu Meya, Songoro Mnyonge na watendaji wa Manispaa hiyo
Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuph Mwenda (mbele) akikagua mto Ng’ombe uliopo eneo la Mwananyamala Kisiwani, wakati wa ziara hiyo Nyuma yake ni Naibu Meya. Songoro Mnyonge.


MEYA wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuph Mwenda amewataka wakazi kwenye mikondo ya maji 
wahame haraka kwa usalama wa maisha yao na si kusubiri waondolewe kwa nguvu.Mwenda alisema tayari baadhi ya wakazi wa maeneo hayo walishalipwa fidia na kutafutiwa maeneo mengine na Serikali lakini wamerejea na kuendelea na maisha yao jambo ambalo alisema sasa Manispaa yake haitasita kuwaondoa kwa nguvu.Akizungumza wakati wa ziara yake aliyoifanya katika maeneo ya mabondeni na mikondo ya maji katika Manispaa hiyo Dar es Salaam jana Meya huyo alisema anashangaa kuona watu wanajenga makazi katikati ya mkondo wa maji na kusababisha maji hayo kukosa uelekeo na kuingia kwenye makazi yaw engine hususan kipindi hiki cha mvua ilhali tayari walishaondolewa.“Mfano watu wa Kinondoni Hananasif na Suna tayari walishapewa fidia na kupewa viwanja, lakini wengi wao wameshauza viwanja hivyo na kurudi tena maeneo hayo. Hii inashangaza sana. Tunafanya hivi kwa faida ya maisha yao hatutaki kuona watu wanakufa yanapotokea mafuriko.” Alisema Meya Mwenda.Mwenda alifanya ziara hiyo katika Kata za Makurumla, Tandale, Makumbusho na Mwananyamala na kushuhudia baadhi ya wakazi wakiwa wamejenga nyumba zao katikati ya mikondo ya maji na kusababisha maji kukosa uelekeo na kuingia katika makazi ya watu ikiwemo Mtaa wa Kimamba eneo la Daraja la Mwinyi.Katika hatua nyingine Meya huyo alimwagiza Mhandisi Mkuu wa Manispaa hiyo kuwasiliana na Wahandisi wa kampuni ya ujenzi ya Strabag kupata ufumbuzi wa tatizo la mifumo ya majitaka inayopita kwenye  barabara hiyo kutafuta njia ya kupeleka maji hayo ili kuzuia yasiingie katika makazi ya watu hususan katika kipindi hiki cha mvua.Hata hivyo Meya huyo amesifu jitihada za wataalamu wa Manispaa hiyo kwa kushirikiana na watendaji za kuhakikisha wanasafisha njia za maji ikiwemo mitaro ma mito mbalimbali akitolea mfano Mto Ng’ombe uliopo Mwananyamala Kisiwani ambao awali ulikuwa ukifurika maji na kusababisha mafuriko maeneo mbalimbali ikiwemo Tandale kwa Mtogole kutokana na kujaa taka ukilinganisha na sasa.Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuf  Mwenda alifanya ziara yake katika maneo mbalimbali ya mabondeni na kwenye mikondo ya maji yaliyopo kwenye Manispaa hiyo Dar es Salaam jana ili kuona athari za mafuriko zilizojitokeza kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha jijini kwa lengo la kutafuta ufumbuzi wa kuepukana na mafuriko hayo.

No comments:

Post a Comment