OFISA
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Philip
Saliboko, amepinga kuhojiwa na Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma na baadala
yake amekimbilia Mahakama Kuu kuweka pingamizi.
Saliboko anatuhumiwa
kupokea mgao wa sh. milioni 40.4 kutoka kwa mmiliki wa kampuni ya VIP
Engineering and Marketing Limited, James Rugemalira, kinyume cha sheria ya
maadili ya viongozi wa umma.
Mgao wa fedha
hizo zinadaiwa kuwa ni sehemu ya fedha zaidi ya sh. bilioni 300 zilizochotwa
kifisadi kutoka akaunti ya Tegeta
Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Hatua ya
‘kukimbilia’ Mahakama Kuu jana, ilichukuliwa baada ya Jaji Hamisi Msumi,
kutupilia mbali pingamizi la awali la kuzuia malalamiko hayo kusikilizwa na
baraza hilo, yaliyowasilishwa na Saliboko kupitia Wakili wake, Jamhuri Johnson.
Wakili
Jamhuri aliwasilisha pingamizi hilo baada ya Wakili wa Sekretarieti ya Maadili
ya Viongozi wa Umma, Hassan Mayunga, kuwasilisha malalamiko hayo dhidi ya Saliboko
mbele ya baraza hilo na kuzua malumbano ya kisheria yaliyodumu takribani dakika
30 kati ya mawakili wa pande mbili.
Wakili
Jamhuri aliwasilisha pingamizi hilo baada ya Saliboko kukana malalamiko yote
yaliyowasilishwa na Wakili Mayunga dhidi yake.
Akiwasilisha
pingamizi hilo, Wakili Jamhuri alidai baraza halina uwezo wa kusikiliza
malalamiko dhidi ya mteja wake kwa madai kwamba kuna amri ya zuio iliyotolewa na Mahakama Kuu
kwa chombo chochote cha umma kushughulikia suala lolote linalohusu kampuni ya
kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) pamoja linalohusu
akaunti ya Tegeta Escrow.
Alidai
zuio hilo lilitolewa kupitia kesi ya msingi namba 5 ya mwaka 2014
iliyofunguliwa na IPTL na wenzake dhidi ya Waziri Mkuu na wenzake saba na
kwamba, baraza lina nakala ya amri hiyo.
Hatua
iliyochukiliwa na Saliboko ni kama ile iliyochukuwa na mbunge wa Bariadi
Magharibi, Andrew Chenge alipofikishwa mbele ya baraza hilo zaidi ya wiki moja
iliyopita.
Hata hivyo,
wakati Wakili Jamhuri akiendelea kutoa hoja kutetea pingamizi la mteja wake,
Jaji Msumi aliingilia kati na kumweleza kuwa katika shauri dhidi ya Chenge,
waliona baraza lina uwezo wa kusikiliza kwa sababu baraza si sehemu ya
waliopewa amri hiyo ya zuio na Mahakama Kuu.
Kauli ya Jaji
Msumi ilijibiwa na Wakili Jamhuri, ambaye alidai amri ya zuio hilo inavihusu
vyombo vya umma na kwamba, baraza ni chombo cha umma, ambavyo vimezuiwa
kuendelea kushughulikia suala hilo hadi kesi hiyo ya msingi iliyopo Mahakama
Kuu itakaposikilizwa na kuamuliwa.
Hoja
hizo za Wakili Jamhuri zilipingwa na Wakili Mayunga, ambaye alidai baraza
limeshaamua pingamizi kama hilo, hivyo haliwezi kuwa na mamlaka tena
ya kuamua.
Wakili
Mayunga pia alidai kwa mujibu wa katiba ya nchi, Sekretarieti ya Maadili ya
Viongozi wa Umma ni idara inayojitegemea na kwamba, amri ya zuio hilo la
Mahakama Kuu si ya dunia nzima na kwa hiyo, haifanyi kazi dunia nzima.
Hoja
hizo za Wakili Mayunga zilipingwa na Wakili Jamhuri, ambaye alidai suala la
Saliboko haliwezi kufananishwa na la Chenge kwa kuwa bado halijaongelewa katika
baraza na kwa hiyo, uamuzi wa baraza wa kutupa pingamizi, unaweza kufanya kazi
katika shauri la Chenge na siyo kwa mteja wake (Saliboko).
Hata
hivyo, Wakili Jamhuri hakukubaliana na uamuzi Jaji Msumi wa kutupilia mbali
pingamizi la mteja wake, hivyo akaliomba liruhusu waende Mahakama Kuu kuomba
marejeo, ili kupata tafsiri sahihi juu ya amri ya zuio hilo.
Jaji
Msumi alikubaliana na ombi hilo la Wakili Jamhuri na hivyo, akaamua kusitisha
usikilizaji wa malalamiko dhidi ya Saliboko hadi ombi la marejeo ya amri ya
zuio hilo la mlalamikiwa litakapotolewa uamuzi na Mahakama Kuu.
Awali,
akiwasilisha malalamiko katika baraza hilo dhidi ya Saliboko, Wakili Mayunga,
alidai Saliboko alikiuka sheria ya maadili ya viongozi wa umma kwa kuomba
fadhila za kiuchumi kutoka kwa Rugemalira.
Alidai
mlalamikiwa alipokea zaidi ya Sh milioni 40.4 zilizoingizwa kwenye akaunti yake
iliyofunguliwa katika Benki ya Mkombozi, tawi la St. Joseph, jijini Dar es
Salaam Februari 5, mwaka jana.
Wakili
Mayunga alidai Saliboko, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Rita, aliteuliwa na
Mahakama Kuu kuwa Mfilisi wa muda wa mali za IPTL, iliyokuwa na mkataba na
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), ambalo ni taasisi ya umma la kuongeza
uzalishaji wa umeme nchini.
Alidai
kitendo cha mlalamikiwa kupokea fedha hizo kutoka kwa Rugemalira, ni ukiukwaji
wa sheria ya maadili ya viongozi wa umma.
Wakili
Mayunga alidai pia kuwa mlalamikiwa alijipatia manufaa ya kifedha na hakutamka
fedha hizo kwa mujibu wa sheria.
Uamuzi
wa Munujangoma
Kwa upande
mwingine, baraza hilo limekubali pingamizi la kutosikiliza kesi ya Mkurugenzi wa Huduma za
Sheria katika Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Rogonzibwa
Mujunangoma.
Mujunangoma alifikishwa mbele ya baraza hilo akidaiwa kujipatia
manufaa ya kifedha kiasi cha sh milioni 423.4 kwa ushauri anaoutoa katika
Kampuni ya VIP na Mabibo Wines and Spirit kinyume cha Sheria ya Maadili ya
Viongozi wa Umma.
Pingamizi hilo lilikubaliwa jana
na Mwenyekiti wa Baraza hilo Jaji Msumi, alisema kuwa baraza limepitia
hoja za msingi za mlalamikiwa na kujiridhisha.
Jaji Msumi alisema hoja ambayo imeonekana kuwa na msingi wa kisheria
iliyochangia kulishawishi baraza kukubali pingamizi hilo ni ukweli kwamba
Mujunangoma amefunguliwa mashitaka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
ambayo ndiyo yale waliyomfungulia katika baraza la maadili.
“Sheria inakataa mshtakiwa akiwa na kesi katika sehemu mbili kwa wakati
mmoja yenye malengo yale yale kwenye vyombo tofauti inamkosesha nafasi ya
kujitetea,” alisema.
No comments:
Post a Comment