MKUU wa Kitengo cha Miundombinu na Nishati kutoka Shirika la
Maendeleo la Taifa (NDC), Pascal Malesa amesema kuwa serikali inatarajia
kutumia Dola za Marekani Milioni 132 kwa ajili ya kukamilisha mradi wa
kuzalisha umeme wa upepo wenye uwezo wa Megawati 50 ifikapo mapema mwaka
2016.
Malesa aliyasema hayo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Nishati na Madini iliyofanya ziara ya kutembelea mradi wa kuzalisha
umeme kwa njia ya upepo unaojengwa katika eneo la Kisesile nje kidogo ya
Singida Mjini.
Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ipo mkoani Singida
kwa ajili ya kukagua miradi ya umeme ili kujionea maendeleo yake pamoja
na kuzungumza na wananchi.
Alisema mradi huo unatekelezwa kwa ubia kati ya Shirika la
Maendeleo la Taifa (NDC) lenye asilimia 60, Shirika la Umeme Nchini
(Tanesco) lenye asilimia 20 na kampuni ya Power Pool East Africa Limited
yenye asilimia 20 chini ya kampuni ya ubia iitwayo Geo Wind Power
Tanzania Limited (Geo Wind) iliyoundwa mwaka 2011.
Malesa alieleza kuwa gharama hizo zinahusisha utekelezaji wa
mradi huo awamu ya kwanza kwa ajili ya kuzalisha megawati 50 ambayo
itahusisha ujenzi wa msongo wa umeme wa kilovolti 220 umbali wa kilomita
12 na kuunganisha kwenye gridi ya taifa.
Alisema fedha hizo ni mkopo kutoka Benki ya Exim ya China na
kuongeza kuwa kwa sasa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) linafuatilia
mkopo huu chini ya udhamini wa Serikali kupitia Wizara ya Fedha baada ya
kukamilisha vigezo vyote vya mradi vilivyotolewa na benki hiyo kwa
ajili ya kupata mkopo wa masharti nafuu na kuviwasilisha benki ya Exim
ya Serikali ya watu wa China.
Alieleza kuwa baada ya Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya
Fedha kuwasilisha maombi ya mkopo kwenye Benki ya Exim ya China mwaka
2013, ujumbe wa kwanza kutoka benki hiyo uliwasili Tanzania mapema Machi
2014 na kufanya uhakiki wa awali wa mradi.
Alisema pamoja na uhakiki wa mradi huo, ujumbe huo ulifanya
mazungumzo na Wizara ya Fedha na wanahisa wa mradi na kuongeza kuwa
ujumbe wa pili kutoka Benki ya Exim ulifika Tanzania mapema Mei, 2014 na
kufanya uhakiki wa kina wa mradi ikiwa ni pamoja na kutembelea eneo la
mradi mkoani Singida na kufanya mazungumzo na uongozi wa mkoa wa
Singida.
Akielezea hatua iliyofikiwa kuhusu mkopo, Malesa aliieleza
kamati kuwa baada ya Serikali kupitia NDC kutimiza masharti yote ya
mkopo na Benki ya Exim kutoka China kufanya uhakiki wa mradi, benki hiyo
iliridhia kutolewa kwa mkopo wenye masharti nafuu tangu mwezi Septemba
mwaka jana kwa ajili ya ujenzi wa mradi huu.
Aliongeza kuwa hivi sasa Serikali kupitia Wizara ya Fedha iko
katika majadiliano ya masharti ya mkopo na kusisitiza kuwa NDC
inafuatilia majadiliano hayo ili kuhakikisha kuwa yanasainiwa mapema ili
kuanza ujenzi mara moja ili kuendana na Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa
(BRN), ambao umeeleza wazi kuhusu lengo la serikali kutekeleza na
kukamilika kwa mradi huu mwaka 2016.
Akielezea matarajio ya mradi huo Malesa alisema mara baada ya
kukamilika kwa mradi huo, mradi utaimarisha uwezo wa Gridi ya Taifa hasa
wakati wa kiangazi kwa kuzalisha umeme wa uhakika na hivyo kusaidia
uhifadhi bora wa maji katika bwawa la Mtera na hivyo kupunguza makali ya
mgawo wa umeme nchini.
No comments:
Post a Comment