![]() |
| Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu |
KAMATI ya Bunge, Ardhi, Maliasili na Mazingira, imesema itapigana kufa na kupona kuhakikisha kodi katika vifaa vya ujenzi vinapunguzwa ili wananchi wamudu kununua nyumba zinazouzwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Ahadi hiyo imetolewa wiki iliyopita na Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Abdulkarim Shah, wakati wa uzinduzi wa ununuzi wa nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), zilizopo maeneo ya Victoria jijini Dar es Salaam.
Shah alisema nyumba zinazouzwa na NHC zimekuwa ghali kutokana na kodi ya vifaa inayotozwa na serikali.
Alisema kutokana na bei kubwa ya nyumba hizo wananchi wengi wamejenga imani kuwa NHC linawalenga zaidi watu wenye vipato vikubwa.
“Tunataka nyumba za NHC ambazo zina ubora mkubwa ziwanufaishe Watanzania wote, tutapambana bungeni ili kodi inayotozwa kwenye vifaa vinavyotumiwa na shirika hili zipunguwe au ziondolewe,” alisema.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu, alisema uzinduzi wa mradi huo ni safari ya mwendelezo kwa miradi mingine ya shirika hilo inayolenga kuwanufaisha Watanzania wote.
Mchechu alisema miradi inayotekelezwa na NHC inaangalia mahitaji ya watu wenye kipato cha chini, kati na juu.
Alisema nyumba hizo zilizopo Victoria zina huduma mbalimbali za kijamii zikiwamo benki, hoteli na sehemu za kuchezea watoto.
Naye Mkurugenzi wa Uendelezaji Biashara wa NHC, David Shambwe, alisema nyumba ya vyumba viwili zinauzwa kwa sh. milioni 165, vyumba vitatu inauzwa sh. milioni 291 na nyumba ya vyumba vinne vinauzwa sh. milioni 306.
Alisema eneo la mradi kuna huduma ya maji safi na salama, jenereta itakayotumika wakati umeme ukizimika, kamera kwa ajili ya kuangalia usalama wa eneo hilo na huduma nyingine muhimu.

No comments:
Post a Comment