KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Sunday, 8 March 2015

SUMAYE: AMANI NI MUHIMU KATIKA UBORESHAJI DAFTARI LA WAPIGA KURA

Waziri Mkuu wa zamani, Sumaye
WAZIRI Mkuu Mstaafu Fredrick Sumaye amesema kuwa taifa linahitaji kuwa na amani na utulivu wakati wa uandikishaji wa wapiga kura katika daftari la wapiga kura, wakati wa kampeni , pamoja na wakati wa kutangaza matokeo.

Sumaye aliyasema hayo jana Tabora Mjini wakati wa harambee ya ujenzi wa Kanisala Moravian Tanzania Magharibi, wilaya ya Reli ya Kati Tabora,  ambapo alisema kuwa katikia mwaka huu ni muhimu uchaguzi uandaliwe vizuri, ufanyike kwa haki na uwazi na usimamiwe vizuri.

Alisema lengo la uchaguzi ni kupata viongozi wapya wazuri, waadilifu, wapenda na watenda haki na wachapa kazi kwani hayo ndio mambo ya msingi yanayowafanya watu wamwombe Mungu nyakati za chaguzi maana nchi nyingi zimeingia kwenye misukosuko kwa kutokuwa makini nyakati za chaguzi.
“Tunahitaji kumwomba Mungu wetu sana ili uchaguzi wetu upite salama na utuletee viongozi watakaojali maslahi ya watu na siyo maslahi yao binafsi au ya marafiki zao wa karibu. Katika jambo hili kuna mambo kadhaa muhimu ya kufanya kazi, likiwemo kuliombea taifa na kuwa na amani na utulivu,”alisema.

Akizungumzia kuhusu amani, Sumaye amesema kuwa lazima serikali ihakikishe kwa kushirikiana na Tume ya Uchaguzi (NEC) kuwa raia wote wenye kustahili kupiga kura wanaandikishwa katika daftari rasmi la wapiga kura.

Aidhama, nafasi ya kutosha itolewe ili kila mtu apate hiyo fursa ya kuandikishwa kupiga kura. Ni muhimu daftari hilo likawa wazi kwa kila mtu kukagua jina lake na kituo chake cha kupigia kura ili kusiwe na malalamiko ya watu kutokuona majina yao au majina kuwa katika vituo vingine ambavyo haviko karibu nao.

“Pia wakati wa Kampeni Tume ihakikishe kuwa vyama vyote vinapewa haki sawa na wote wanalindwa na sheria na taratibu zilizowekwa. Vyombo vya dola vihakikishe kampeni ni za utulivu na fujo zozote zinadhibitiwa na wavunja amani wanaadhibiwa bila kujali umaarufu wao wala wa vyama wanakotoka,”alisema.

Alisema hatua hiyo inatokana na kushuhudiwa watu wakienda kwenye mikutano ya kampeni na silaha za moto au za jadi hali ambayo inasababisha watu kukatwa mapanga, mashoka na nondo. 

“Vyama vya siasa vinatakiwa viwaelimishe watu wao kuwa siasa si uadui wala mapambano ya silaha bali ni kushindana kwa hoja. Vyombo vya dola katika eneo hili vinatakiwa vifanye kazi bila huruma mradi vinafuata sheria. 

Sote tukumbuke kuwa hakuna chama chochote wala kiongozi yeyote aliye juu ya sheria,”alieleza.

Kuhusu udanganyifu katika kuhesabu kura na kutangaza matokeo, Sumaye alisema kuwa hilo ni eneo nyeti na kama uwazi wa kutosha haupo fujo na umwagaji damu huweza kutokea.

No comments:

Post a Comment