![]() |
| Makamu wa Rais, Dk. Bilal |
HEKTA 400,000 za misitu zimekuwa zikipotea kila
mwaka kutokana na uelewa mdogo wa wananchi katika kutumia rasilimali hizo bila
kuzingatia matumizi endelevu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais
(Mazingira), Dk. Binilith Mahenge, alitoa kauli hiyo wakati akimkaribisha
Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, katika uzinduzi wa Ripoti ya pili ya
hali ya Mazingira nchini ya mwaka 2014, uliyofanyika jijini Dar es Salaam jana.
Alisema, uharibifu huo umechangiwa na kutozingatiwa
sheria na kanuni za hifadhi ya mazingira katika ngazi mbalimbali.
“Suala la sera, sheria na kanuni za hifadhi ya
mazingira kutozingatiwa katika ngazi mbalimbali kumechangia pia katika uharibifu
wa mazingira nchini,”alisema Dk. Mahenge.
Dk. Mahenge, alisema takwimu za uchomaji moto
hovyo kwa kipindi cha mwaka 2000 hadi 2014 zimeonesha kwamba, katika kipindi hicho kumekuwa na matukio ya
uchomaji moto takriban hekta 1,123,000.
Aliitaja mikoa iliyoathirika na moto huo kuwa ni
Rukwa, Kigoma, Tabora, Mbeya, Ruvuma, Lindi na Morogoro.
“Kwa mfano asilimia 50 tu ya miji mikubwa ina
mifumo ya majitaka amabayo inahudumia asilimia nane tu ya wakazi wa miji hiyo
hali hii inachangia kwa kiasi kikubwa cha uchafuzi wa mazingira,”alisema Dk.
Mahenge.
Dk. Mahenge, alisema athari nyingine
zinazotokana na uchafuzi wa mazingira ni pamoja na; kuonezeka kwa magonjwa ya
mlipuko kama vile kuhara damu na kipindupindu ambayo huchangia asilimia 60 hadi
80 ya matukio ya magonjwa na kiongezeka kwa gharama za kutibu maji ya kunywa.
Aliongeza kwa kusema kuwa uharibifu wa rutuba ya
ardhi umechangia uvunaji hafifu wa mazao katika mikoa ya Dodoma, Shinyanga,
Tabora na Singida.
Dk. Mahenge, alisema uharibifu huo wa ardhi
umechangia pia kuongezeka kwa migogoro ya ardhi inayohusisha jamii za wafugaji
na wakulima, ambayo imesababisha maafa makubwa katika jamii hizo ikiwemo vifo.
Aliyataja baadhi ya maeneo yaliyokumbwa na
migogoro hiyo ni Rufiji mkoani Pwani, Kilosa na Kilombero (Morogoro), Kiteto
(Manyara) na Mbarali (Mbeya).
Naye Dk. Bilal,
alisema uharibifu wa mazingira katika nchi zinazoendelea ni kati ya sababu
zinazofanya nchi hizo ziendelee kuwa masikini.
Alisema uko uhusiano mkubwa kati ya mazingira na
umasikini kwa maana ya kwamba uharibifu wa mazingira unachangia kuongezeka kwa
umasikini, hivyo kadri ya hali ya umasikini inavyoongezeka inasababisha pia
kuharibika kwa mazingira.
“Kwa maana hiyo umuhimu wa kulinda na kuhifadhi
mazingira nchini unachochewa zaidi na ukweli kwamba mazingira ni muhimu sana
katika ustawi wa maisha yetu,”alisema Dk, Bilal.
Aidha, mazingira ni mhimili wa sekta za
uzalishaji kama vile kilimo, utalii, uvuvi na madini.
Dk. Bilal, alisema changamoto iliyoko ni
kuhakikisha mazingira na maliasili hizo zinatumka katika njia endelevu kwa
kuzingatia uwiano mzuri.

No comments:
Post a Comment