NAIBU Waziri wa Maendeleo ya Jamii
Jinsia na Watoto Mheshimiwa Dkt. Pindi Chana amefanya ziara ya
kutembelea Mahakama ya watoto na Mahabusu ya watoto za Jijini Dar es
salaam. Mheshimiwa Naibu Waziri alifanya ziara hiyo kwa lengo la
kuangalia maeneo ambayo yanahitaji maboresho pamoja na kujionea hali
halisi ya uendeshaji wa kesi zinazohusu makosa ya wototo na jinsi watoto
wanavyohifadhiwa katika Mahabusu hiyo.
Katika ziara hii Mheshimiwa Naibu
Waziri aliwasili katika Mahakama ya Watoto iliyopo ndani ya majengo ya
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es salaam saa mbili asubuhi
siku ya tarehe 21Aprili 2015. Akiwa katika Mahakama hiyo ya Watoto
aliweza kuhudhulia uendeshwaji wa kesi kadhaa ikiwemo usikilizwaji wa
kesi tatu zinahusu makosa ya watoto.
Ambapo kesi ya kwanza ilihusu
ubakaji wa mtoto wa kiume dhidi ya mtoto wa kike ambapo ilikuwa katika
hatua ya kusomewa maelezo ya awali, kesi ya pili pia ilihusu ubakaji
ambayo ilikuwa katika hatua ya utetezi wakati katika kesi ya tatu nayo
ilihusu ubakaji katika hatua ya kusikiliza ushahidi upande wa mashitaka.
Mheshimiwa Naibu Waziri
alifanikiwa pia kufika katika Mahabusu inayotumika kuhifadhi watoto
wakati wakisubiri kesi zao kusikilizwa na watoto ambao kesi zao
zimeishaisha. Mahabusu hiyo iliyopo Upanga jijini Dare es salaam
inashikilia jumla ya watoto 35, wasichana wakiwa ni wanne (4) na
wavulana 31 wenye umri kuanzia miaka 11 hadi 17.
Tanzania bara ina mahabusu za
watoto sita (6), ambazo zinatumika kama vituo vya maadilisho ya watoto.
Mahabusu hizo zipo mikoa ya Dar es salaam, Tanga, Kilimanjaro, Arusha,
Mbeya na Mtwara. Mahabusu hizi zinatumika kuhifadhi watoto kutokana na
sababu mbalimbali zinazohusiana na kesi zao. Sababu hizo ni pamoja na
mtoto kukosa dhamana au mdhamini, mtoto kutengwa na hivyo kukosa ndugu
au jamaa wa karibu wakati kesi yake ikisubiri tarehe husika na aina ya
kosa ambalo halina dhamana, kama kesi za mauaji.
Ziara hii ya Mheshimiwa Naibu
Waziri iliweza kubaini mambo mengi kuhusiana na masuala ya watoto.
Miongoni mwa masuala yaliyobainika ni kwamba, kesi nyingi za watoto
zinahusu ulawiti wa watoto wa kiume kwa wenzao wa kiume au wa kike,
mauaji na wizi.
Aidha katika kutekeleza haki ya
mtoto ya Kusikilizwa Mheshimiwa Dkt. Pindi Chana alikutana na watoto
katika Mahabusu hiyo iliyopo Upanga Jijini Dar es salaam ili kusikiliza
maswali, maoni na changamoto zinazowakabili. Watoto hao (majina
yanahifadhiwa kwa sababu maalum) walijieleza kwa kina kesi zinazo
wakabili na hali waliyonayo katika mahabusu hiyo, ambapo wengi
walilalamikia ucheleweshwaji wa kesi zao kwa upande wa Mahakama na
Upande wa Jamuhuri ambaye ndiye mshitaki, hali inayowafanya washindwe
katika muda kushiriki katika masomo na kuungana na familia zao.
Mheshimiwa Naibu Waziri ameishauri
jamii hasa wazazi na walezi kusimamia malezi sahihi ya watoto na kuacha
kupuuza mambo yanayohusu malezi na makuzi ya watoto. Akiongea kuhusiana
na makosa ya watoto Dkt. Pindi Chana amekemea zaidi suala la wazazi na
walezi kuwafundisha watoto mambo ya kikubwa kabla ya umri wao kufika kwa
kuwa kesi nyingi zinazo kabili watoto zimeonekana ni za Ubakaji au
Ulawiti, Mauaji na wizi kwa kutumia silaha.

No comments:
Post a Comment