KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Sunday, 12 April 2015

MFUMO WA KAMERA UNAHITAJIKA BAADALA YA TOCHI KUDHIBITI MADEREVA WAHUNI

Mbunge wa Moshi Mjini, Ndesamburo

MBUNGE wa Moshi mjini Philemon Ndesamburo ameitaka serikali kuweka mfumo wa kamera ambao utakaosaidia kudhibiti madereva wanaokwenda kinyume na sheria za usalama barabarani na kusababisha vifo vya Watanzania wasikuwa na hatia.

Ndesamburo, alitoa kauli hiyo baada ya kuisikia taarifa kwenye vyombo vya habari kuwa serikali imeondoa utaratibu wa tochi barabarani kwa vile ulikuwa ni miongoni mwa madai ya madereva wakati walipogoma wiki iliyopita.

Katika mgomo huo madereva walikuwa wakidai kuwa wamechoka kufanyakazi bila ya mikataba inayoeleweka, kutolipwa mishahara na wengine kulipwa kwa utaratibu wa huduma za simu jambo ambalo linaikosesha mapato serikali.

Kingine ni utaratibu wa tochi wawapo safarini, kikubwa ambacho wanapinga ni utaratibu wa kutakiwa kwenda kusoma tena kila baada ya miaka mitatu wanapobadilisha leseni zao ambapo pia walidai kuwa ada ya sh. 560, 000 ya mafunzo hayo ni kubwa, kwamba wao ni vibarua hawana uwezo wa kupata fedha hizo.

Wakati akijibu kero za madereva hao juzi Waziri, alisema kuwa serkali imeyapokea matatizo yao na kwamba utaratibu wa kurudia kusoma umefutwa, tochi barabarani hakuna na vituo vituo vya ukaguzi vitatumika vya mizani tu.

Akizungumza na mwandishiwa habari hizi, kwa njia ya simu, Mbunge huyo alisema hakubaliani na uamuzi wa kuondolewa tochi barabarani kwani kwa kufanya hivyo ajali zitaongezeka zaidi.


“Tanzania watu wanakufa kila siku kutokana na madereva kwenda mbio, sasa huyo waziri kuondoa tochi unadhani atapunguza ajali au watu waendelee kufa? Sasa huyo waziri kuondoa tochi ina mana anataka watu waendelee kufa, mimi sikubaliani naye,”alisema Ndesamburo.

Alisema hivyo kwa mfumo wa tochi umeshindwa kufanyakazi kutokana na wasimamizi wake kuugeuza mfumo huo kuwa mradi wa rushwa barabarani hivyo kupoteza imani kwa madereva.

Alisema mfumo huo watochi umelalamikiwa kutokana na waliokabidhiwa dhamana kushindwa kuwatendea haki madereva hivyo kuufanya uonekane kuwa haufai.

Ndesamburo alisema kutokana na mazingira hayo ni vema serikali ikaanzisha mfumo wa kamera ambao unatumika katika nchi mbalimbali zilizoendelea.

“Naamini utaratibu wa kuweka kamera unawezekana, nchi hii fedha zipo, kama watu walijichotea fedha za Escrow walivyotaka iweje washindwe kuweka kamera, inawezekana kabisa,”alisema Nesamburo.

Kuhusu elimu, Ndesamburo alisema elimu haina mwisho na ndio maana hata wazee leo wanasoma, hivyo hakubaliani na uwamuzi wa kufuta mafunzo ya madereva, kwa vile ulimwengu wa sasa ni wa sayansi na teknolojia hivyo kunakuwa na madiliko ya mara kwa mara katika matumizi ya vyombo mbalimbali katika kila sekta.

Alisema ziandaliwe sheria ambazo zitaleta tija kwa walengwa huku kila tajiri ambaye ameamua kuajiri akubali kulipa gharama za mafunzo ya dereva wake, wazingatie kwamba elimu ni msingi wa kila kitu duniani.











No comments:

Post a Comment