KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Sunday, 12 April 2015

WATANZANIA WAISHIO NJE HAWATAWEZA KUPIGA KURA

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na Watanzania waishio Uingereza kwenye makazi ya Balozi wa Tanzania nchini humo, Aprili 11, 2015. Kulia kwake ni Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Peter Kallaghe. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)



WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amesema Watanzania waishio ughaibuni hawataweza kupiga kura wakiwa nje ya nchi kwenye uchaguzi wa Oktoba mwaka huu.

Pinda alitoa kauli hiyo juzi alipozungumza na baadhi ya Watanzania waishio Uingereza kwenye makazi ya Balozi wa Tanzania nchini humo, Balozi Peter Kallaghe, yaliyoko Highgate, Kaskazini mwa Jiji la London.

Alisema mambo makuu yanayohitaji kuzingatiwa kabla hawajaweza kupiga kura ni marekebisho ya sheria ya uchaguzi namba 1 ya mwaka 1985 pamoja na uandikishwaji wa Watanzania wana-Diaspora kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

"Najua suala kubwa ambalo mnatamani kulisikia ni hili la Watanzania kuweza kupiga kura kutokea huku mliko. Hili inawezekana lisifanikiwe wakati huu kwa sababu kuna mambo muhimu ya kuzingatia kubwa likiwa ni marekebisho ya sheria.
“Pia ili mwananchi aweze kupiga kura ni lazima awe ameandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura," alisema.

Alisema wanaangalia kama mashine za BVR nazo zitapaswa kupelekwa kwenye kila ubalozi, ili watu waweze kujiandikisha au itafutwe njia nyingine ya kufanikisha hilo jambo.

“... lakini watu wa tume wanaamini kwamba jambo hilo linaweza kufanikiwa kwenye uchaguzi wa mwaka 2020," alisema.

Waziri Mkuu ambaye aliwapatia nakala zisizopungua 40 za Katiba Inayopendekezwa, alitumia fursa hiyo kuwasisitizia wasome kwa makini Katiba hiyo ili wawe na uelewa mpana.




No comments:

Post a Comment