KURUGENZI ya Mawasiliano Ikulu imesema hakuna sababu ya kumzuia Rais Jakaya Kikwete asitie saini miswada ya Sheria ya Makosa ya Matumizi mabaya ya Mitandao na Sheria ya Takwimu kwa kuwa imepitia hatua zote muhimu hadi kupitishwa na Bunge.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya
Ofisi ya Rais Ikulu, Salva Rweyemamu, alisema Rais Kikwete atatia saini ili kuifanya
kuwa sheria na iwapo kutakuwa na matatizo yanaweza kujadiliwa baadaye.
“Kama tunakubaliana kuhusu ukubwa wa matatizo hasa ya ugaidi, mambo
mengi ya ugaidi yanapitia katika mitandao.
Ni wazi kwamba hapa kwetu sheria hii imechelewa sana, kwa sababu
imefikia hatua watu wanatumia mitandao hii kutukanana, kudhalilishana na
kunyanyasana.
Rais atatia saini na kama kuna tatizo, marekebisho yatafanyika
baadaye,” alisema.
Alisema ni wazi kwamba sheria hizo hazikulenga kuminya wala kupunguza
uhuru wa habari na mawasiliano katika mitandao ya simu na intaneti bali
kinachofanyika ni kuweka udhibiti kwa watumiaji, hasa wale wenye nia mbaya ya
kutumia visivyo mitandao hiyo, kwa faida ya umma.
Alisema haitakuwa mara ya kwanza kwa sheria hiyo kupitishwa na
kufanyiwa marekebisho, kwa kuwa zipo baadhi ya sheria zilizowahi kufanyiwa
marekebisho katika baadhi ya vipengele vyake.
Salva alieleza kwamba katika hili, usalama wa nchi ndilo suala namba
moja, huku masuala mengine yanayohusu uhuru wa habari yakifuatia, kwa kuwa bila
usalama hakuna uhuru wa jambo lolote.
Akizungumzia kuhusu sheria ya vyombo vya habari, alisema serikali
ililazimika kusikiliza kilio cha wadau japokuwa ni kweli kwamba muswada huo
ulioanza miaka 10 iliyopita umeshapita kwenye mikono ya wadau mara nyingi.
Alisema serikali inatambua kwamba miswada ya sheria za habari zimekuwa
zikikandamiza uhuru wa habari, ndiyo maana imeendelea kusisitiza umuhimu wa
kupata sheria mpya itakayotoa uhuru zaidi kwa vyombo hivyo na wanahabari.
Ziara ya Rais
Jordan
Akizungmzia ziara ya siku moja ya Rais Kikwete nchini Jordan, alisema
ujumbe wake ulikwenda nchini humo Aprili 18, mwaka huu kwa mwaliko wa Mfalme
Abdulla ili kushiriki katika mkutano wa viongozi wa kidunia uliohusu masuala ya
usalama, ulinzi na namna ya kudhibiti ugaidi, ambao ulipaswa kuwa siri.
Alisema ofisi yake haikutoa taarifa kuhusu safari hiyo ya Rais kwa
kuwa Jordan iliomba mkutano huo uwe siri kutokana na nchi hiyo kuzungukwa na
nchi ambazo si salama, ikiwamo Syria, Iraq, Palestina, Saudia, Israel na Misri.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amesema Muswada wa Sheria
ya Takwimu uliopitishwa na Bunge hivi karibuni hautawazuia watafiti kufanya
tafiti zao kwa ajili ya matumizi yao na taifa.
Waziri Mkuu Pinda alitoa kauli hiyo kutokana na wasiwasi ulioonyeshwa
na watafiti kuhusu Muswada wa Sheria ya Takwimu uliopitishwa na Bunge pamoja na
Sheria ya Makosa ya Mtandaoni wakati wa kongamano lililoandaliwa na Ofisi ya
Taifa ya Takwimu (NBS).
Akizungumza katika kongamano hilo lililoanza jana jijini Dar es Salaam
na kuwakutanisha wataalamu wa Sekta ya Takwimu wa Bara la Afrika, Pinda alisema
sheria hiyo inatokana na mtazamo wa dunia kuwa eneo hilo linapaswa kusimamiwa
na vyombo vya serikali.
Waziri Mkuu Pinda alisema sheria hiyo
imetengenezwa kutokana na mifumo ya mazingira ya nchi nyingine duniani,
lakini zikijitokeza changamoto huko mbele ya safari kuna uwezekano wa
kuboreshwa ili kwenda na wakati.
“Takwimu zinazotolewa lazima ziwe na viwango vya kimataifa kwa ajili
ya yeyote atakayezitumia, awe na uhakika, tena bila ya kuhoji,” alisema.
Akizungumzia kongamano hilo, Waziri Mkuu Pinda alisema
limezikutanisha nchi zinazozungumza lugha ya Kiingereza na Kifaransa.
Alisema lengo lake ni kuendeleza msukumo wa kuzitaka serikali zote za
nchi zinazoendelea kwa kutoa msukumo wa kipaumbele katika sekta hiyo ya
takwimu.
Alisema nchi inapokuwa na takwimu sahihi inaweza kupanga mipango yake
ya maendeleo kwa uhakika zaidi.
Waziri Mkuu Pinda alisema serikali itaijengea uwezo taasisi yake ili
iweze kutoa takwimu zenye ubora na viwango vya kimataifa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Albina Chua, alisema taasisi zote nchini
zinaruhusiwa kufanya utafiti lakini lazima ziwe na viwango vinavyotakiwa ili
zitumike katika kupanga maendeleo ya nchi.
CHANZO TANZANIA DAIMA
CHANZO TANZANIA DAIMA

No comments:
Post a Comment