NA MWANDISHI WETU
KAMPUNI ya upakiaji na upakuaji wa mizigo bandarini (TICTS), inatarajiwa kutumia sh. bilioni 30 mwaka huu kwa ajili ya upanuzi wa miundombinu yake ikiwemo ununuzi wa mitambo miwili ya kisasa.
Mtendaji Mkuu wa TICTS, Paul Wallace, alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa hatua hiyo inalenga kukabiliana na ongezeko kubwa la mizigo inayopitia Bandari ya Dar es Salaam.
Mitambo hiyo miwili yenye uwezo wa kubeba hadi makontena 15 kila moja kwa wakati mmoja, itagharimu sh. bilioni 20 na itafika nchini ndani ya miezi 12.
“Tunafanya kila linalowezekana kuhakikisha tunaboresha miundombinu yetu na tulifurahishwa sana na ujio wa Rais Jakaya Kikwete na marais wenzake kutoka nchi jirani.
Hii inatupa imani kwamba tunafanya kitu kinachoheshimika na kutangaza kwa majirani zetu kwamba bandari yetu ni salama na yenye ufanisi mkubwa,” alisema Wallace.
Alibainisha kuwa kampuni hiyo kwa sasa ina mitambo mikubwa minne na inashusha makontena takriban 500,000 kwa mwaka. Idadi hiyo imekuwa ikiongezeka kwa kiwango cha kati ya asilimia 10 na 12 kwa mwaka.
No comments:
Post a Comment