KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Friday, 3 April 2015

ABIRIA WAPTA JOTO YA JIWE BAADA YA KUFUNGA BARABARA YA MSIMBAZI/KARIAKOO

Mafundi wa Kampuni ya Ujenzi Strabag wakiwa kazini

KUFUNGWA kwa Barabara ya Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es Salaam juzi, kumesababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji wa barabara hiyo.

Tanzania Daima juzi ilishuhudia watu wakitembea kwa miguu umbali mrefu huku wakishindwa kutambua vituo vipya vya kupandia daladala.

Barabara hiyo imefungwa kutokana na kujengwa upya kwa ajili ya mradi wa mabasi yaendayo haraka ambayo inaishia kwenye kituo kikuu kinachoendelea kujengwa eneo la Kamata.

Baadhi ya madereva waliozungumza na mwandishi kwa nyakati tofauti,  walisema kufungwa kwa barabara hiyo kutasababisha msongamano eneo la Kariakoo.

Dereva anayeendesha daladala zinazoelekea Kimara, John Mushi, alisema kujengwa kwa barabara ni jambo zuri, lakini tatizo ni ujenzi wenyewe kuchukua muda mrefu.

 “Hawa jamaa ujenzi wao sijui vipi! Wanabomoa hapa, pale na kule lakini kujenga inawachukua muda mrefu, sasa bora wangekuwa wanavunja eneo ambalo wanakusudia kujenga tu ili eneo jingine tulitumie,” alisema Mushi.

Hata hivyo pamoja na kufungwa huko baadhi ya magari yatapata unafuu kutokana na kipande cha barabara kilichoanzia kwenye makutano ya Mkunguni na Msimbazi hadi kwenye makutano ya Uhuru na Msimbazi yanaruhusiwa kupita kila upande wa barabara hiyo isipokuwa katikati ya barabara. 

Eneo la Katikati ya barabara limekwanguliwa lami yote na kuanza kuchimbwa kwa ajili ya ujenzi.

Mmoja wa abiria aliyejitambulisha kwa jina la  Asha Said, alisema abiria wengi wanasumbuka kwani maeneo waliyozoea kupanda magari hayatumiki kutokana na ujenzi na inachukua muda hadi kujua yako wapi.

Daladala zilizohamisha vituo ni zile za Buguruni, Sinza, Manzese na Muhimbili, ambapo baadhi vimehamia mitaa ya Mkunguni, Mafia na Tandamti.



No comments:

Post a Comment