KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Friday, 3 April 2015

VIJANA WAKWAMA BANDARINI WAKISAFIRI KWENDA ZBR



Baadhi ya vijana waliyokwama bandarini wakienda Zanzibar

KUNDI la vijana 35 waliokuwa wakisafirishwa kwenda kufanya kazi za mashamba Zanzibar leo walikwama bandarini baada ya kukosa usafiri.

Muonekano wa vijana hao wenye umri kati ya miaka 16 hadi 30 ulikuwa hauna tofauti na ule wa vijana waliokuwa wakikamatwa nchini wakitokea katika nchi za Ethiopia, Somalia na Eretria.

Vijana hao ambao wametoka Shinyanga, Simiyu, Mwanza, Tabora na Geita walikwama bandarini hapo baada ya kukosa tiketi kutokana na meli zote kujaa abiria ambao walikuwa wakienda Zanzibar kwa ajili ya  mapumziko ya Sikukuu ya Pasaka.

Kiongozi wa kundi hilo, Mangu Zizi, alisema hawakuweza kusafiri kama walivyokusudia kwa sababu walikuwa hawajakata tiketi mapema na waliambiwa kuwa wangesafiri baada ya siku tatu.
“Hata hivyo, tuliambiwa kama tunataka kusafiri leo tutoe sh. 50,000 kila mmoja wakati sisi tuna sh. 25,000 kwa kila mmoja wetu.
“Tumefika hapa tangu asubuhi hadi sasa  (mchana) hatujakula chochote kutokana na hela tulizo nazo ni kidogo na tukikosa usafiri kabisa tutakwenda kulala Kituo cha mabasi Ubungo,” alisema Zizi.

Zizi alisema imekuwa ni kawaida kwa vijana wa Kanda ya Ziwa kusafiri kwenda Zanzibar na kwamba wakifika watatawanyika kwa wengine kwenda Pemba na wengine kubaki Unguja.
Zizi alimtaja mwenyeji wao kuwa ni Kassim Kolofwa, ambaye ndiye atakayewapokea wakati watakapofika Zanzibar.

Hata hivyo, alipotafutwa Kolofwa kwa njia ya simu jana alisema kati ya vijana hao anaowafahamu  kuwa ni vijana wake ni watatu ambao ni Mangu Zizi na mdogo wake Jitu na mwenzao na kusema kuwa wengine hawatambui.

Alisema vijana hao wanapofika huko wanafikia kwa sheha na kukabidhisha vitambulisho vyao kwa ajili ya kupata kibali cha kuendelea kuishi visiwani humo.

Kolofwa alisema hiyo si mara ya kwanza kwa vijana kutoka Bara kwenda Zanzibar kwa ajli ya kufanya kazi za vibarua mashambani.
Usafiri wa Kwenda Zanzibar tangu juzi umekuwa mgumu hadi kufanya baadhi ya abiria kulalamikia hali hiyo.

No comments:

Post a Comment