KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Wednesday, 29 April 2015

WAMILIKI WA REDIO WATAKIWA KUJENGA TASWIRA NJEMA


Meneja wa kituo cha Redio Jamii FADECO ya wilayani Karagwe, Adelina Lweramula akichangia hoja wakati wa mafunzo hayo yaliyomalizika jana kwenye kituo cha Redio Jamii Sengerema-Telecentre mkoani Mwanza.
Mwandishi wetu, Mwanza

WAMILIKI wa redio za jamii wametakiwa kujenga taswira njema za redio zao ikiwa wanataka redio zao zitamanike na kutumiwa na wadua mbalimbali wa maendeleo nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Mwezeshaji wa warsha ya Viongozi wa vituo vya redio jamii Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wakati (ASMET), Ramadhan Ahungu.
Akizungumzia malengo ya warsha hiyo na madhumuni yake alisema kwamba kuwapo kwa mpango wa biashara ndani ya redio hizo hakutakuwa na maana kama wasipozingatia ujenzi wa taswira utakaowafanya wadau kuvutiwa na redio hizo.
Alisema kuna umuhimu wa suala hilo kwani kusipojengeka kwa mahusiano bora kati yake na jamii, watu binafsi na taasisi za kiraia zenye malengo tofauti katika kuhudumia wananchi, redio hizo hazitakuwa na biashara ya kufanya.
Ahungu pamoja na kusifia mtindo uliotumika kuwezesha redio hizo kuandaa mipango kazi ya biashara yenye lengo la kusimamia masoko na fedha alisema warsha imefanikiwa kuwaweka karibu zaidi na wadau wamiliki wa vyombo hivyo.
Warsha hiyo ni hitimisho ya awamu ya kwanza kwa ufadhili wa mradi wa Shirika la Maendeleo la Sweden (SIDA) wa kuzipa uwezo redio za jamii katika matumizi ya Tehama na mawasiliano inayoratibiwa na Shirika la Kimataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni UNESCO iliyofanyika katika kituo redio cha Sengerema Telecentre mkoani Mwanza.
Alisema katika warsha hiyo wamiliki hao walijifunza uandaaji wa mipango ya biashara, kutunza fedha, utafutaji masoko, uhakiki wa mipango ya biashara na vipindi vya redio kwa lengo la kuona namna ya kuvifanya kuleta biashara.
Naye Meneja wa kituo cha Redio Jamii Kahama FM ya Shinyanga, Marco Mipawa akizungumzia mafunzo hayo alisema yamemsaidia sana katika kuhakikisha kwamba kituo chake kinakuwa bora na kinachovutia watangazaji.
Alisema mafunzo hayo yamewafanya wajitambue kwani yamefanyika mfululizo kwa mara 5 na kuwafanya wabadilike.
Aidha Meneja wa kituo cha Redio Jamii FADECO ya wilayani Karagwe, Adelina Lweramula alisema kwamba anashukuru mafunzo kwa kuwa yamewafanya kuondoa mawazo vichwani na kuweka mipango kazi katika karatasi na kuwezesha wafanyakazi nao kufuatilia.



No comments:

Post a Comment