Rai hiyo imetolewa na mkuu wa
wilaya ya Temeke Sophia Mjema wakati akifunga mafunzo ya elimu ya afya
ya uzazi, ujinsia na stadi za maisha kwa wanafunzi na walimu wa shule
za sekondari za wilaya hiyo iliyopo mkoani Dar es Salaam.
Mjema alisema mimba za utotoni ni
moja ya kikwazo cha kuleta maendeleo katika jamii hivyo basi kila
mtu hana budi kuhakikisha anatokomeza tatizo hilo.
“Vijana hasa wanafunzi ni kundi
linalokabiliana na mabadiliko makubwa katika miili yao mabadiliko ambayo
huwaweka katika hatari kubwa ya kukumbwa na matatizo ya kujamiiana na
kupata mimba katika umri mdogo, vifo vitokanavyo na uzazi, utoaji mimba
na magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya kujamiiana ikiwa ni pamoja na
Ukimwi”.
Nawaomba sana mzingatie yale
mliyojifunza ili muweze kukabiliana na tatizo la mimba za utotoni ambalo
ni janga la taifa letu. Mimba za utotoni zinasababisha kuongezeka kwa
umaskini katika jamii ikiwamo kukosa huduma muhimu, kukosekana kwa
wasomi kwani watoto wa kike hushindwa kuendelea na masomo”, alisema
Mjema.
Mkuu huyo wa wilaya alisema mimba
za utotoni zinasababisha kuongezeka kwa watoto wa mitaani, kuongezeka
kwa vijana tegemezi na kushamiri kwa uhalifu, kuhatarisha maisha ya mama
na mtoto wakati wa kujifungua na watoto kukosa baba maalum na malezi
bora.
Kwa upande wake Meneja
Uraghibishi na Mawasiliano kutoka Taasisi ya Wanawake na Maendeleo
(WAMA) Philomena Marijani alisema mafunzo hayo ni mwendelezo wa shughuli
ya uzinduzi wa kampeni ya jilinde utimize ndoto yako iliyofanyika
mwishoni mwa mwaka jana katika viwanja vya Taasisi hiyo jijini Dar es
Salaam na kuzinduliwa na Mke wa Rais na Mwenyekiti wa WAMA Mama Salma
Kikwete.
Philomena alisema, “Taasisi ya
WAMA ina dira ya kuwawezesha wanawake na wasichana ili wawe na maisha
bora kwa kufanya juhudi kuhakikisha wasichana na wanawake wanakuwa na
maendeleo ya kielimu, afya na uchumi kwani tatizo hili la mimba ni moja
ya sababu inayowarudisha nyuma kimaendeleo wasichana wa kike wasiweze
kufikia ndoto zao”.
Akisoma hotuba kwa niaba ya
Mkurugenzi Mkuu wa Mradi wa Engenderhealth Tanzania Richard Killian,
Dkt. Martha Kisanga ambaye ni Meneja wa Kanda ya Pwani aliipongeza
Serikali kwa mchango wake katika kuendeleza elimu ya afya hususan afya
ya uzazi kwa vijana kwa kuweka mikakati na sera kwa ajili ya kuhakikisha
vijana wanapata malezi na elimu bora ya afya ya uzazi.
Dkt. Martha alisema iwapo mikakati
hiyo itatekelezwa kwa umakini itasaidia kuhakikisha vijana wetu
wanapata elimu bora ya afya ya uzazi ili kuepuka mimba zisizotarajiwa,
utoaji wa mimba ovyo, magonjwa ya zinaa na Ukimwi na kujiepusha na
vitendo vinavyohatarisha maisha yao.
“Nichukue nafasi hii kuhakikisha
sisi wadau wa maendeleo tuko bega kwa bega na Serikali ili kutekeleza
mikakati ya sera zinazohusu vijana, Taasisi yetu itaendelea kushirikiana
na wilaya ya Temeke na zingine zitakazopendekezwa na WAMA kupitia Idara
ya Afya ya Elimu kuhakikisha kwamba vijana wengi zaidi wanafaidika
kutokana na elimu hii ambayo itakuwa endelevu”, alisema Dkt. Martha.
Mafunzo hayo yako chini ya mradi
wa kuzuia mimba za utotoni katika shule za sekondari unaotekelezwa na
Taasisi ya WAMA na Engenderhealth kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo
la watu wa Marekani yalihudhuriwa na wanafunzi 65 na walimu 11 kutoka
shule za Sekondari za Kibasila, Minazini, Miburani, Kurasini, Aboud
Jumbe, Chang’ombe, Tandika, Keko, Lumo, Buza na Mbagala.
Mada zilizofundishwa ni
uelimishaji rika, mila na desturi zinazoathiri Afya ya uzazi kwa vijana
na elimu ya Afya ya uzazi itolewayo shuleni na katika vituo vya afya,
ujinsia, stadi za maisha, dhana ya ushauri na unasihi, elimu ya magonjwa
ya ngono, Ukimwi, njia za kujikinga na mimba za utotoni na mamna ya
kupanga matumizi ya muda katika saa.

No comments:
Post a Comment