KARATA ya Kiongozi wa
ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, kwenye ulingo wa siasa Mkoani hapa ilichezwa
kwa kumbukumbu ya kuwapigania wanachi wa Kahama kwenye sakata la mkataba tata
wa mgodi wa dhahabu wa Buzwagi.
Akiwahutubia wakazi wa mji wa Kahama kwenye viwanja ya CDT, Zitto alisema wanachi
wa mji huo wanayo kila sababu ya kumuunga mkono kwenye harakati za kisiasa kwani
aliwapigania bila kujali kuwa yeye ni mbunge wa wapi.
Akizungumza kwa uchungu wakati akieleza namna
aliyoshughulikiwa na bunge mara baada ya kupeleka hoja binafsi ya mkataba tata
wa mgodi wa buzwagi na serikali ambao alidai kulikuwa na wizi mwaka 2007.
Kabwe, amesema baada ya sakata hilo alizunguka nchi nzima
na ndio tukio ambalo hawezi kulisahau na mkoa huo umekuwa wa historia ya
kisiasa kwake.
“Misukosuko niliyopata katika ulingo wa kisiasa katika muda
wote na hassa mwaka mmoja uliopita umenimfanya niwe na moyo wa chuma wa
kuwapigania watanzania, Ujasiri wa kuwapigania watanzania kwangu ulianza wakati wa
sakata la Buzwagi mwaka 2007 tukio lililoniweka katika ramani ya wanasiasa
makini,” Alisema Zitto.
Alisema pamoja na kupitia katika misukosuko ya kisiasa ikiwemo
kutoungwa mkono na wabunge wenzake na hata kusababisha kusimamishwa
kutohudhuria vikao vya Bunge bado alisimama imara na kuhakikisha watanzania
wanajua uovu wa iongozi wa serikali ya Chama cha Mapinduzi(CCM).
Aliongeza kuwa kwake Kahama ni mji wa kihistoria kwa kuwa hoja yake kuhusu mgodi wa Buzwagi ndio imemtangaza
kisiasa ambapo kabla ya hapo alikuwa kama mwanasiasa mwingine yeyote nchini.
“Niliwasilisha hoja katika Bunge ya tisa na kulitaka Bunge
kufanya uchunguzi wa mapitio ya mikataba ya madini hasa kwa kuundwa Kamati
Teule ya Bunge kuchunguza mapitio ya Mikataba ya Madini na mazingira ya
kusainiwa kwa mkataba mpya wa madini wa Buzwagi.
Zitto
ambaye kabla ya kuacha kuwa mbunge mwezi mmoja
uliopita alisema mkataba wa Buzwagi ulisainiwa na aliyekuwa Waziri wa
Nishati na Madini wa wakati huo Nazir Karamagi, huko Uingereza
Februari 2007.
“Kuletwa kwa hoja hiyo, bila kujali maamuzi ya kuhusu hoja
yenyewe, ilikuwa ni ishara tosha ya ukomavu wa demokrasia ndani ya Bunge ila
pamoja na yote nilisimama kutetea haki za wana Kahama lakini nikakosa uugwaji
mkono.
Zitto ambaye pia aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati
ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), alisema hatua ya Serikali kusaini mkataba
huo mgodi wa Buzwagi kati ya na Kampuni
ya Barrick alisimama kuhoji sababu za
mkataba huo kusainiwa nje ya nchi, London Uingereza.
Alisema pamoja na kutoungwa kwake mkono bado asimama kwa ajili ya kutetea Taifa na watu
wake ili liweze kunufaika na rasilimali za Taifa ikiwemo kuwekwa kwa mazingira
mazuri ya mikataba ya madini ambayo watawanufaida Watanzania wote wakiwemo
wanaozunguka migodi ya madini.
Kuhusu madai kuwa ameingia katika Chama cha ACT wazalendo
kwa ajili ya kuwaandalia njia watu wengine wagombee Urais Zitto alisema
wanaojenga hoja hiyo wameishiwa na mambo ya kusema na kwamba hatahangaika
kuwajibu.
Alisema ACT wazalendo wana miiko ya uongozi na kwamba
yeyote anayetaka uongozi ndani ya chama hicho atalazimika kufuata miiko hiyo.
“Wanaosema hatuhangaiki nao ila wajue sisi tuna miiko ya
uongozi na yeyote atakayekuja ajue kuwa ana wajibu wa kuifuata miiko hiyo ya
maadili”alisema Zitto
Kuhusu kugawa kura za wapinzani Zitto, alisema Chama hicho
hakipo kwa ajili hiyo bali kazi yake ni kuwatafuta watanzania zaidi ya asilimia
58 walioacha kupiga kura katika uchaguzi uliopita
Alisema katika uchaguzi wa mwaka 2010 waliojiandikisha kwa
ajili ya kupiga kura walikuwa watu milioni 20 na kwamba waliopiga kura walikuwa
milioni 8.
Zitto alisema ni wakati wa watanzania kuwaunga mkono watu
wanaowapigania kimaslahi pasipo kujali anatoka eneo gani la nchi na kwamba
maslahi ya Taifa hayana mipka katika kusimamiwa.
Awali Mwenyekiti wa Chama hicho Anna Mghwira, alisema ni
jambo la kusikitisha kuona watanzania wanashindwa kusimama katika hoja za
kimaendeleo na badala yake wanasimama katika kusikiliza uzushi.
Alisema jukumu la kuhakikisha CCM inaondoka madarakani ni
jukumu la watanzania wote na kwamba hakuna chama chenye mamlaka ya
kujimilikisha hali hiyo ya kuwapigania watanzania kutoka katika makucha ya
kidhalimu.
Katika mkutano huo baadhi ya vijana walijaribu kufanya fujo
kabla ya mkakati wao huo kudhibitiwa na wananchi waliojitokeza kwa wingi katika
mkutano huo.
No comments:
Post a Comment