KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Thursday, 23 April 2015

WATANZANIA WAMETAKIWA KUSAIDIA JAMII ILIYOTENGWA KUTOKANA NA WAATHIRIKA WA DAWA ZA KULEVYA

WATANZANIA nchini wametakiwa kusaidia jamii iliyotengwa kutokana na sababu mbalimbali wakiwemo watoto yatima, waathirika wa dawa za kulevya , wajane na wazee ili kupunguza tatizo la ukosefu wa maadili katika jamii.
Wito huo umetolewa jana na mlezi wa kituo cha kusaidia vijana walioathirika na dawa za kulevya linalojulikana kwa jina la SAWODAYO la Kaloleni Jijini Arusha Mary Kimambo  wakati akipokea msaada wa vyakula vya aina mbalimbali kutoka kampuni ya usagishaji nafaka ya Monaban.
Kampuni hiyo ilikabidhi katoni 20 za unga wa ngano, katoni  20 za unga wa mahindi, gunia la maharage, mafuta ya kupikia, na  sabuni za kufulia na kuogea ambavyo vyote vina thamani ya zaidi ya sh 3 milioni.   
Alisema kwa sasa kituo hicho ambacho kinahudumia vijana wapato 62 kimeelemewa kutokana na idadi ya vijana hao kuwa kubwa ikilinganishwa na uwezo wa kituo kuwahudumia hivyo analazimika kuomba msaada kwa wananchi wenye mapenzi mema na nchi yao .
“Tuliamua kusaidia vijana hawa ambao mwanzo walikuwa wachache tofauti na sasa, lengo letu ilikuwa kusaidia vijana ambao ni ndugu na jirani zetu ambao walijiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya lakini sasa tumepanua wigo wa msaada wetu na tunahudumia vijana kutoka maeneo mbalimbali”alisema mlezi huyo
Naye Mkurugenzi wa kampuni hiyo Philemon Mollel wakati akitoa msaada huo aliungana na mlezi huyo katika kuikumbusha jamii wajibu wao wa kibinadamu wa kuwasaidia wasiojiweza.
“Tunasaidia sio kwasababu tunao uwezo na ziada katika biashara yetu, hapana bali tunaguswa na mahitaji ya wananchi wenzetu ambao kutokana na sababu mbalimbali walijikuta hivyo walivyo, hatutakiwi kuwatenga bali kuwasaidia”
 Aliishauri serikali ambayo kila mwaka katika bajeti yake inatenga fedha kwa ajili ya makundi kama hayo ihakikishe fedha hizo zinawafikia walengwa badala ya kuishia mikononi mwa watu wachache ambao wanajinufaisha wao binafsi.
“Fedha zinazotengwa kwaajili ya makundi haya zikitumika vizuri zitasaidia kupunguza tatizo , na sisi wananchi wengine tukishikana na kuungana na vikundi kama Sawodayo kusaidia pale tunapoweza , basi  nchi yetu itakuwa mahali salama pa kuishi na kufanya kazi za maendeleo”alisema Mollel

No comments:

Post a Comment