KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Sunday, 7 June 2015

ANNA: LAZIMA WANAWAKE WAWEZESHWE KATIKA ELIMU YA UJASIRIAMALI

Mwakilishi wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Anna Mtaita.

ILI mtoto aweze kukua katika mazingira mazuri, ni lazima wanawake wawezeshwe kwa kupewa elimu ya ujasiriamali.
Kauli hiyo ilitolewa  mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam  na mwakilishi wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Anna Mtaita, wakati wa uzinduzi wa Albam ya kuelimisha jamii juu ya mtoto inayoitwa  ‘Thamani Yetu  Leo’uliofanyika Kijitonyama.
Akizungumza katika uzinduzi huo ambao umepambwa na vikundi mbalimbali vya burudani vikiwemo ngoma za asili, Sarakasi na maigizo, Mtaita alisema ili watoto waweze kufikia malengo yao kuna haja elimu ya ujasiriamali kutolewa tangu shule ya awali.
“Mtoto ni mtu wa thamani kubwa katika taifa lolote hivyo  aendelezwe  kwa kupewa elimu  ya ujasiriamali  tangu akiwa shule ya awali ili atakapokuwa  mkubwa akute fursa mbalimbali zitakazomuwezesha kumudu maisha yake”alisema Mtaita.
Akizungumzia kuhusu ongezeko la watoto wa mitaani, Mtaita alisema chimbuko la watoto hao ni kutokana na familia nyingi kuwa na maisha duni.
Awali mwakilishi kutoka asasi isiyokuwa ya kiserikali ya Women In Society 
(WOINSO) ambayo ndiyo iliyozindua albam hiyo, Janeth Mwasawala alisema, wameamua kuzindua albam hiyo,  kwa kuzingatia changamoto mbalimbali ambazo watoto wanakutana nazo na kufanya washindwe  kutimiza ndoto zao.
“Watoto wanaambukizwa magonjwa ya ngono, kwa makusudi,wanakatishwa maisha yao hasa walemavu wa ngozi (Albino) na mimba za utotoni.”alisema.
Mwasawala alisemamradi huo wa ‘Thamani Yetu Leo’ unalenga kuwafaidisha  moja kwa moja watoto kwa kuwapa thamani yao wanayostahili kwa haki zao za msingi zikiwemo haki ya kuishi,haki ya kusomeshwa ,kusikilizwa na kusaidiwa.
Aliongeza kuwa uzazi usio na mpango umechangia kwa kiasi kikubwa kuwa na watoto wengi ambao wanakosa haki zao za msingi kutokana na uwingi wao katika familia ikizingatiwa na hali halisi ya Uchumi wa familia hiyo.
“Elimu inahitajika kwa kiasi kikubwa ili kunusuru janga la watoto wa mitaani ambao wanaweza kukimbia familia zao na kwenda mtaani pindi wanapokosa mahitaji yao ya msingi”alisema. Mwasawala.


No comments:

Post a Comment