WAZIRI wa Kilimo, Chakula
na Ushirika, Stephen Wassira amewaeleza Watanzania kuwa wawe makini na baadhi
ya viongozi wala rushwa wanaotaka urais, kuigeuza Ikulu kama kijiwe cha
walashwa.
Wassira, aliyasema hayo jana
wakati akitangaza nia ya kuomba ridhaa ya kugombea urais wa awamu ya tano kupitia
Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika ukumbi wa B.o.T ulioko jijini Mwanza.
Alisema amekuwa kiongozi
katika awamu zote lakini hajawahi kuwa na kashfa ya wizi akitolea mfano wizi wa
EPA na Tegeta Escrow ambapo zote hizo jina lake halikutajwa kwamba hakuhusika.
Wasira, alisema kama Ikulu
atawekwa kiongozi mpenda rushwa, kunauwezekano, kiongozi huyo akweza kuja kuuza
mipaka nchi.
“Mimi sio mwizi kama ningekuwa
mwizi ningeweza kuwaiba hata mbolea yenu pale Wizarani,”alisema Wasira.
Wasira, alisema kuna baadhi
ya watu wamekuwa wakiizungumzia rushwa fasheni wakati hakuna wa kupinga kuhusu
tatizo hilo ambalo limekuwa hadi kuifanya ikose maendeleo.
“Mimi sio mla rushwa na
kuna baadhi ya watu mkiwaona wananozungumzia tatizo rushwa hebu jaribuni
kuwapima kama kweli inawakera, kwani kuna wengine walizungumzia tatizo la
rushwa kama fasheni lakini haliwaumizi.
“Mwalimu Nyerere aliwahi kusema,
mtu anayekerwa na rushwa akizungumzia tatizo la rushwa muangalieni
machoni…nimeitumikia Tanzania katika awamu zote lakini kwenye kashfa ya EPA
sikutajwa na hata ya Esrow sikutajwa pia, na sio kama siwezi kuiba, ningeiba
hata mbolea zenu kwasababu najiamini.
Mwalimu Nyerere alishawahi
kuniambia, Wassira unahitaji uongozi au utajiri? Kama unataka utajiri nenda
kafanye biashara. Kama umepata baada ya kuwa Waziri basi moja kwa moja wewe
utakuwa ni mwizi, kwasababu mshahara wa mwisho wa mwezi hauwezi kukutajirisha,
biashara hauna halafu unatajirika huu ni wizi.
“…alisema mtu kama huyu
aogopewe kama ukoma, hivyo Ikulu hatuwezi kuweka mla rushwa, mkiweka mla rushwa
siku nyingine atauza Ikulu yenu,” alisema Wassira.
Akielezea vipaumbele vyake endapo
atachaguliwa kuwa rais, alisema atahakikisha kuwa naimarisha bandari ya Tanga
na Dar es Salaam pamoja na kutengeneza barabara ikiwemo ile ya kutoka Dar es
Salaam hadi Chalinze.
“Awamu ya nne imefanya mambo
makubwa vizuri katika suala la kutengeneza barabara, zilizobaki zitatengenezwa,
tutashirikiana na sekta binafsi katika kujenga kutoka Tanzania mpaka Kigali na
kwasasa tunampango wa kuanza kutengeneza barabara kutoka Dar es Salaam hadi Chalinze na badala ya hapo tutaendelea na nyingine,”
alisema Wassira.
Wasira, alisema katika rasilimali
za taifa, serikali lazima ichukue hatua, katika kuwasaidia wachimbaji wadogo
ili waweze kuondokana na migogoro na pia zisaidie kupambana na umaskini na
zitumike kwa faida ya kila mmoja.
Alipoulizwa swali na
mwandishi wa habari wa Raia Mwema kuhusu wizi uliopo serikalini na ripoti mbaya
za Mkaguzi na Mdhibiti wa hesabu za Serikali (CAG), Wasira alisema ufike wakati
mkaguzi huyo apewe madaraka kisheria kwamba anatakapowabaini wezi haina haja ya
kufikish ripoti kwa rais, bali aagize wakamatwe na kufikishwa mahakamani.
Alisema atahakikisha kuwa
atakapokuwa rais mambo hayo yanasafishwa kabisa na hakuna atakayesamehewa
katika hilo.

No comments:
Post a Comment