KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Thursday, 16 July 2015

CCK WAKOSOA UTEUZI WA DK. MAGUFULI KAGAME

Dk. Magufuli
KITENDO cha Shirikisho la Soka Tanzania(TFF), kumtangaza mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Kombe la Kagame, kimezidi kuibua hisia tofauti miongoni mwa wadau katika jamii.
Wengi wao wanahoji mantiki ya Rais wa Shirikisho hilo, Jamal Malinzi, kufanya hivyo katika kipindi hiki ambacho vyama vya siasa vipo katika mchakato wa kupata wagombea wao katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Chama Cha  Kijamii (CCK), Renatus Muhabhi, alisema uamuzi wa Malinzi na TFF yake si sahihi, kwani ni sawa na kuanza kumpigia debe.
Alisema kwa mazingira yalivyo, Dk. Magufuli ataitumia nafasi hiyo kuanza kujipigia debe na chama chake, jambo ambalo si haki, kwani wengine bado hawajapata fursa hiyo.
“Dk. Magufuli hafahamiki kimataifa, hivyo anatengenezewa mazingira
ya kuanza kujinadi kupitia michuano ya Cecafa inayoshirikisha nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati,” alisema.
Muhabhi, alisema hivi sasa kuna upotoshaji mkubwa unaofanywa na CCM wa kuwaaminisha wananchi kuwa, mgombea huyo kama vile tayari ni rais, wakati bado ni mgombea sawa na wa vyama vingine.
“Niwaombe wananchi wakipuuze chama hicho cha CCM kwa kumfanya mteule huyo kama tayari ni rais, tunapinga kumpa ulinzi kama Rais wa nchi, pia tunataka wakati wa kampeni ndipo wapewe ulinzi,” alisema.
Muhabhi, ametoa wito kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, kuwazuia wagombea waliothibitishwa na vyama vyao na tume hiyo kujinadi
kabla ya kipindi maalumu cha kampeni.
Juzi TFF kupitia kwa Ofisa Habari wake, Baraka Kizuguto, ilimtangaza Dk. Magufuli kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa michuano hiyo na kuibua mikanganyiko na hisia za kisiasa miongoni mwa wadau wa michezo, wakihusisha na kampeni za kisiasa kwenda kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba.

Aidha, baadhi ya wadau hao walielezea TFF kujiingiza kwenye kampeni za kisiasa kutaathiri maendeleo ya mchezo huo hapa nchini.

No comments:

Post a Comment