KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Tuesday, 21 July 2015

TUMIENI MITANDAO KUPANUA MASOKO

Prof. Kamuzora
WATANZANIA wametakiwa kutumia mitandao ya kijamii kupata taarifa mbalimbali na kuzitumia katika maendeleo.
Mjumbe wa Bodi ya Utendaji ya Kituo cha Ushirikiano wa Kilimo na Maendeleo Vijijini cha nchi za Umoja wa Ulaya, Afrika, Karebiani na Pasifiki (CTA), Prof. Faustin Kamuzora, alisema taarifa hizo zina mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta za kilimo, usindikaji, biashara na ukuzaji wa masoko katika ukanda wa Afrika Mashariki na dunia nzima kwa jumla.
Akifungua mafunzo ya mawasiliano ya mitandao ya kijamii jijini Dar es Salaam jana, alisema kuna kila sababu kwa Watanzania kutumia mitandao hiyo kuchochea shughuli za uzalishaji na biashara.
“Mitandao hii imekuja kutuongezea tija...inaokoa muda.  Ikitumika vyema ina faida kubwa,” alisema Kamuzora ambaye pia ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe anayeshughulikia Utawala na Fedha.
CTA na Baraza la Nafaka la Afrika ya Mashariki (EAGC) wanashirikiana kutoa mafunzo kwa wajumbe kutoka taasisi mbalimbali kwa ajili ya kuwezesha matumizi ya mitandao ya kijamii.
Aliwataka wanasemina hao kupitia ujuzi watakaoupata kuusambaza katika taasisi zao na kuwa tayari kuwapa wananchi taarifa juu ya hali ya hewa, masoko na bei ya mazao ya nafaka, na mifugo kupitia mitandao kama blogu, facebook na twitter.
Pia aliwataka wanapotumia mitandao hiyo wakumbuke kufuata sheria inayoongoza katika sekta hiyo ndogo.
Kwa upande wake, Meneja Miradi wa EAGC, Ikunda Terry, alisema baraza lao limeamua kuandaa mafunzo hayo kwa kushirikiana na CTA kuwaleta wadau mbalimbali wanaojihusisha na teknolojia hiyo kuwafundisha namna ya kupeleka ujumbe na elimu kwa jamii.

Wajumbe 30 kutoka taasisi mbalimbali nchini wananufaika na mafunzo hayo ya wiki nzima.

No comments:

Post a Comment