![]() |
| Guninita |
ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es
Salaam, John Guninita amesema ni kosa kwa mwanachama wa chama hicho kupinga
uamuzi wa mkutano mkuu na vikao vingine
vya ndani ya chama kwani ni utovu wa nidhamu.
Kauli hiyo ya Guninita inatafsiriwa kuwa ni sawa na kuipa kisogo kambi
ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ambayo hadi sasa imekuwa ikipinga uamuzi
wa vikao vilivyompitisha mgombea urais kupitia chama hicho, Dk. John Mgufuli.
Hivi karibuni mwanasiasa mkongwe na kada wa CCM mwenye kadi namba 8,
Kingunge Ngombale-Mwiru ambaye amekuwa ni miongoni mwa watu wa karibu wa
Lowassa, alipinga mfumo uliotumika kuwachuja wagombea wa urais kupitia CCM.
Kingunge alisema Kamati ya Maadili huko nyuma ilikuwa ni chombo cha
kuandaa taarifa, ili kuisadia Kamati Kuu katika kuwajadili wagombea lakini
katika mchakato wa mwaka huu kamati hiyo imefanya kazi isiyowahusu kikatiba kwa
kukata majina ya wagombea.
Alisema Kamati ya Maadili ya CCM yenyewe imekosa maadili ya kuheshimu
katiba na taratibu za chama.
Alisema kamati hiyo haikuwa na madaraka ya kupeleka majina matano kwenye
kamati kuu, ambayo ilipaswa kuhoji wagombea wote 38 badala yake kuna baadhi ya
watu waliamua kuitumia Kamati ya Maadili kuandaa watu wao na kuwakata wengine
kwa sababu zao.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Guninita alisema kutokana na kanuni za chama
hicho ni kosa kwa mwanachama kupinga uamuzi wa vikao vya chama hicho.
Guninita ambaye alikuwa mmoja wa wanachama waliotia nia kugombea Jimbo
la Kilombero, alisema kamwe yeye kama mwanachama hai wa chama hicho hatapinga uamuzi
wa vikao vya chama.
Alisema ameamua kujitoa kugombea kiti hicho kwa kile anachodai kuna mizengwe
katika kupatikana kwa mgombea ndani ya chama hicho.
“Niliamua kugombea ubunge katika Jimbo la Kilombero, lakini baada ya kutafakari
nimebaini kushinda kwangu ni kazi ngumu mno, nimeamua kujitoa kutokana na
mchakato unavyokwenda lakini bado ni mwanachama halali wa CCM na nitamuunga
mkono mgombea yeyote atakayepita.
“Mtu yeyote atakayepitishwa na chama lazima aheshimiwe, kwani hayo ni
maamuzi ya vikao vya chama, kutoheshimu ni utovu wa nidhamu,” alisema
Guninita.
CHANZO TANZANIA DAIMA

No comments:
Post a Comment