| Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Shaban Mwinjaka |
CHAMA cha Wafanyakazi Madereva nchini (TADWU), kimesema wiki ijayo kitaendesha mafunzo ya siku tano kwa madereva ambao ni wanachama wake ili kupunguza ajali zinazotokea mara kwa mara.
Mafunzo hayo yatakwenda pamoja na kusitishwa kwa huduma za usafiri katika kipindi chote madereva watakapokuwa darasani na uhakiki wa vyeti kwa wahusika utafanyika.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Naibu Katibu Mkuu wa TADWU, Rashid Salehe, alisema wameamua kufanya hivyo kutokana na kamati iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwa ajili ya kuyatafutia ufumbuzi madai ya madereva hao kushindwa kufanya hivyo.
“Tumeamua kwenda kuwapa madereva wetu mafunzo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, popote alipo afahamu kamati aliyoiunda haijamaliza matatizo ya madereva,” alisema Salehe.
Hata hivyo semina hiyo imetafsiriwa na baadhi ya wadau wa sekta ya usafiri kuwa ni mgomo baridi unaolenga kuzorotesha shughuli za usafirishaji nchini.
Akielezea dhana hiyo, Salehe alisema hawafanyi mgomo bali wanawaongezea ujuzi madereva ili kuepusha ajali zinazotokea barabarani, ambazo nyingi zinatokana na baadhi yao kutokuwa makini.
Aliongeza kuwa amesikitishwa na Idara ya Habari (Maelezo) kukizuia chama hicho juzi walipotaka kutoa tamko lao kwa waandishi wa habari katika ukumbi uliopo idarani hapo na unaotumika kwa mikutano mbalimbali.
Wakati TADWU wakitangaza kuendesha mafunzo hayo, Katibu Mkuu wa Chama cha wamiliki wa mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani (TABOA), Ernea Mrutu, alisema hawana taarifa hiyo.
Alisema inaonekana TADWU wana ajenda iliyojificha nyuma na wanayatumia mafunzo husika kutekeleza kile wanachokitaka, ambacho kimsingi kitakuwa na athari kubwa kwa pande zote kama kitafanyika kama inavyosemwa.
“Tunatoa wito kwa madereva wetu ambao tumewaajiri wasijiunge katika semina hiyo na kwa wale watakaojiunga tutawafutia mikataba yao…mtu huwezi kulala leo kesho ukaja ukatuambia unaandaa semina kwa madereva wote, ni lazima kuwepo na utaratibu unaokubalika,” alisema Mrutu.
Mrutu alisema semina hiyo ambayo aliita ni ‘mgomo baridi’, utawapa hasara zaidi wamiliki, kwa kuwa abiria watakaposikia jambo hilo hawatafika vituoni kupata huduma ya usafiri.
Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taboa, Mwesigwa Kazaula, alisema semina hiyo ni mwendelezo wa chokochoko kwa madereva wasiokuwa na kazi wa Chama cha TADWU, na kudai kuwa mara kwa mara wamekuwa wakianzisha migomo batili.
“Tunaomba suala hili lifanyiwe kazi na serikali, maana linaonyesha litaleta athari kubwa kama madereva hao watafanya mgomo huo,” alisema Kazaula.
Naye Katibu Msaidizi wa Chama cha Kutetea Abiria nchini (CHAKUA), Godwin Ntongoji, alisema chama hicho hakijawapa taarifa yoyote, hivyo kukitaka kiandike barua kuhusu kusitisha huduma hiyo ili chama hicho kitoe taarifa kwa wananchi ambao wanataka kusafiri kwa wiki hiyo wasikate tiketi za kusafiria.
Mmoja wa madereva wa Kampuni ya Sumry inayofanya safari kutoka Dar es Salaam kwenda Bukoba, Tumaini Elias, aliliambia Tanzania Daima kuwa amefurahishwa na uamuzi wa Chama cha TADWU kwenda kuwapa semina ambayo itawawezesha waongeze ujuzi zaidi na kutambua haki zao.
No comments:
Post a Comment