WIZARA ya Mambo ya Ndani kupitia Sekretarieti ya Kuzuia na
Kupambana na Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu imezuia zaidi ya
taasisi 70 kusafirisha wafanyakazi wa ndani katika nchi za Uarabuni.
Hatua hiyo inatokana na kushamiri kwa biashara hiyo ambapo
Tanzania inadaiwa kutumika kama njia ya kusafirisha wafanyakazi kwenda mataifa
mengine.
Hayo yalibainishwa jana jijini Dar es Salaam na Katibu wa sekretarieti
hiyo, Separatus Fella wakati wa kutoa mafunzo maalum kwa waandishi wa habari
kuhusu mikakati na mapambano dhidi ya uharamu huo.
Alisema miongoni mwa taasisi ambazo zimezuiwa kufanya biashara
hiyo haramu ni Mtemvu Foundation licha ya kuwa wana vibali halali kuwatafutia
Watanzania kazi katika nchi mbalimbali.
“Hili katazo lilitolewa mwezi uliopita kwa sababu kubwa ya
kushamiri kwa vitendo viovu wanavyofanyiwa Watanzania katika nchi za Uarabuni,
ikiwemo kufanyishwa kazi ngumu na kutumikishwa kingono,”alisema.
Pia alisema hatua hiyo inatokana na taasisi hizo kushindwa kufuatilia
taarifa za wafanyakazi hao pindi wanapokuwa katika nchi hizo, licha ya kuwa
bado wakikabiliana na ‘vishoka’ ambao bado wanafanya biashara hiyo.
Naye Ofisa Mwandamizi wa sekretarieti hiyo, Alex Lupiya
alisema mafunzo hayo yanalenga kutoa elimu kwa Watanzania ili kuzidisha
mapambano dhidi ya biashara hiyo.
Alisema serikali imeridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa na
mwaka 2008 ilitunga Sheria ya Kuzuia Usafirishaji Haramu wa Binadamu ili
kuhakikisha watu wanalindwa.
“Licha ya kushirikiana
na wadau wengine likiwemo Jeshi la Polisi na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
kwa ajili ya kutoa elimu, bado tunakabiliwa na tatizo la fedha kwa ajili ya
kuendeshea semina na vikao,”alisema.
No comments:
Post a Comment