KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Friday, 7 August 2015

WAMACHINGA WAGOMA KUONDOKA JANGWANI

WAFANYABIASHARA ndogo ndogo (wamachinga), walioko katika eneo la Jangwani, wamegoma kuondoka katika eneo hilo kama walivyotakiwa na uongozi wa Halmashauri ya Ilala Julai 30, mwaka huu.
Mwishoni mwa Julai Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) iliutaka uongozi wa manispaa hiyo kuwaondoa wafanyabiashara hao na kusitisha zoezi la kugawa eneo hilo kutokana na kutofaa kwa shughuli zozote za kibinadamu.
Akizungumza na wandishi jijini Dar es Salaam jana, Mhasibu wa Umoja wa wafanyabiashara hao, Pascal Kalo, alisema hawapingani na uamuzi wa serikali bali wanachopinga ni kuondolewa bila ya kupatiwa eneo jingine.
Alisema kuwa wameshindwa kuondoka katika eneo hilo kutokana na uongozi wa manispaa hiyo kushindwa kuwapatia eneo mbadala.
Kalo alisema pamoja na kuwa wako tayari kuondoka katika eneo hilo lakini hawana uhakika na uamuzi huo wa serikali, ndiyo maana waliamua kukimbilia mahakamani kuweka zuio la kutoondolewa katika eneo hilo.
“Pamoja na kuwepo mipango ya kutafutiwa eneo mbadala bado tumekwenda mahakamani ili wakati tukisubiri eneo jipya  tutambuliwe kuwa tupo kisheria zaidi,” alisema Kalo.
Kalo alisema viongozi wa wamachinga hao walikutana na mkuu wa wilaya ambaye aliwataka waorodheshe majina na picha zao ambapo kwa sasa wanafanyia kazi suala hilo.
 “Hata kule watakotupeleka ni lazima watuhakikishi kuwa hakutakuwa na usumbufu tena na hili tutaliweka kisheria,” alisema.
Alipotafutwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Mushi, kuzungumzia kauli hiyo, alisema: “Mpate Mkurugenzi wa  Ilala ndiye anayesimamia utekelezaji wa agizo hilo.”
Naye Msemaji wa manispaa hiyo, Tabu Shaibu, alisema agizo la utekelezaji la kuwataka kuondoka liko pale pale na hivi sasa wanajiandaa na muda wowote watawaondoa wafanyabiashara hao.


No comments:

Post a Comment