WATU watatu wamefariki dunia na wengine 34 wamelazwa katika vituo mbalimbali kutokana
na kuugua ugonjwa wa kipindupindu jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana,
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, alisema chanzo cha ugonjwa huo ni
mkazi wa Ali Maua ambaye alifariki dunia nyumbani kwake Agosti 15 mwaka huu.
“Familia yake ilifanya msiba wa kawaida bila ya kuchukua
tahadhari zozote, matokeo yake familia nzima iliambukizwa,” alisema Makonda.
Alisema watu watatu tayari wamefariki dunia na wengine 34 wamelazwa
katika Hospitali za Mwananyamala na
Sinza.
Alisema watu 18 wakiwamo watoto 14 na wakubwa wanne wamelazwa
katika Hospitali ya Mwananyamala huku Hospitali ya Sinza wagonjwa 16 ambao
watatu ni wanawake na wanaume 13.
Makonda alizitaja kata zilizoathirika na ugonjwa huo kuwa
ni Kijitonyama, Kimara, Saranga,
Manzese, Tandale, Makumbusho na Mwananyamala.
Alisema Manispaa ya Kinondoni imefungua kambi maalumu kwa ajili
ya kuwahudumia wagonjwa katika Zahanati
ya Kijitonyama ambayo ni ya muda yenye uwezo wa kuchukua watu 30 na baadaye
watahamishiwa katika kambi ya Mburahati.
“Sisi kama serikali ya wilaya tumejipanga vizuri
kukabiliana kikamilifu na ugonjwa huo,
kwani tuna dawa na vifaatiba vya kutosha vya kukabiliana na ugonjwa huo.
“Tumefungua kambi yetu katika zahanati ya Kijitonyama ambayo
ina dawa za kutosha na vifaatiba vyote vinayohitajika ,” alisema Makonda.
Makonda alitoa wito kwa wananchi wote kuzingatia kanuni za
usafi ikiwa ni kunawa mikono baada ya kutoka chooni, kuchemsha maji ya kunywa,
kula chakula cha moto na kuwahi mapema hospitali baada ya kuona dalili zozote
za kuharisha au kutapika.
Alisema uzoefu unaonyesha kuwa wagonjwa wengi wanapoteza
maisha kwa kuwa wanafika hospitali kwa kuchelewa hivyo kuwa vigumu kuokoa
maisha yao.
No comments:
Post a Comment