KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Monday, 22 February 2016

POLISI NYAKANAZI WADAIWA KIUSHIRIKI KUPOTEA KWA MBUZI 26



MKUU wa Kituo cha Polisi Nyakanazi wilayani Biharamulo mkoani Kagerea, ameingia matatani baada ya kudaiwa kuhusika katika kuibwa mbuzi 26 kati ya 33, wa mkazi wa kijiji hicho, Daud Kikwaba.
Tukio hilo linadaiwa kutokea Oktoba 12 mwaka jana katika kijiji hicho, baada ya watu wanaodaiwa kuwa wezi kuvamia zizi la mwananchi huyo nyakati za usiku na kuondoka na mbuzi hao.
Akizungumza na mwandishi jijini Dar es Salaam leo, Kikwaba alimtaja Mkuu huyo wa kituo hicho kwa jina moja la Neligwa, ambaye hivi sasa amehamishiwa kikazi kwenye kituo kingiene, anapaswa kutoa taarifa za kusaidia kupatikana mbuzi wake.
Alisema, kuhusika kwake kumetokana na mkuu huyo ni kutoa kibali kwa watu hao wanaodaiwa kuwa wezi ili waweze kusafirisha mbuzi hao, ambao alikuwa akijua fika kwamba walikuwa wa wizi kwani mmoja wa wawezi hao alikuwa anashikiliwa kituoni hapo.
“Kabla ya Mkuu huyo kutoa kibali, wezi hao walikwenda kuomba kibali kwa Menyekiti wa Kitongoji cha Nyakanazi kwa ajili ya kuwasafirisha kusikojulikana lakini mwenyekiti huyo aliwakatalia kutokana na kuwatilia shaka watu hao.
“Mkuu huyo wa kituo anahusika kupotea kwa mbuzi hao 26 kwa vile siyo muadilifu kwani baada ya kubaini kuwa mbuzi wale walikuwa wa wizi kwa hiyo akaona hawana mwenyewe   ndipo alipoamua kushirikiana na wezi hao kuwachukuwa mbuzi hao 26 kisha kubakiza mbuzi saba kituoni hapo,”alisema Kikwaba.
Kikwaba, alisema baada mkuu huyo kukamilisha mchezo huo mchafu, aliamua kumuita kituoni hapo kwa ajili ya kuwatambua mbuzi waliokuwa wakishikiliwa hata hivyo, alipofika alikuta mbuzi saba kati ya 33, huku polisi wa kituo hicho wakimshikilia mtu mmoja kwa madai ya kuhusika na wizi huo.
Hata hivyo, Kikwaba alishangazwa na vitisho alivyopewa na mkuu huyo wa kituo miongoni mwa hivyo ni pale alipolazimishwa kumhudumia mtuhumiwa wa wizi huo kwa kumpeleka hospitali kutibiwa majeraha aliyopata baada ya kushambuliwa na wananchi.
“Nilijaribu kukataa lakini nilipewa vitisho kwamba endapo ningetaa kumhudumia mahabusu huyo kwa kumpeleka hospitali na kupatia huduma ya chakula basi wangenishughulikia kutokana na vitisho hivyo ilinibidi nikubali,”alisema Kikwaba.
Alisema pamoja na yote hayo, mkuu huyo wa kituo aliamua kumuachia mtuhumiwa huyo, kitendo ambacho kimesababisha kukwama kwa kesi aliyofungua Mahakamani Januari mwaka huu.
“Utaona ubabaishaji wa mkuu huyu wa kituo, kwani January 9 mwaka huu alimleta mahakamani mtu mwingine ambaye hahusiki jambo ambalo hakimu aliwataka polisi warudi wakamlete muhusika kwa hiyo hadi leo hawajampeleka hivyo kuendelea kuchelewesha kupatikana haki yangu,”alilalamika Kikwaba.
Alisema, licha ya malalmiko yake hayo kuyafikisha kwa diwani, mbunge na Mkuu wa Wilaya, ambao nao walitoa magizo ya kupatiwa haki yangu lakini cha kushangaza hadi leo polisi hao hawaja chukuwa hatua zozote za kunisaidia zaidi ya vitisho.
Kikwaba, alisema mara ya mwisho, alipofika kituoni hapo alielezwa kuwa asikanyage tena kituoni hapo kwani mhusika hivi sasa amehamishwa kikazi kwenda kituo kingine kwa hiyo mkuu wa kituo aliyopo ni mpya, halifamu shauli hilo.
“Hata Mkuu wa Kituo wilayani Biharamulo anazo taarifa zangu, naiomba serikali inisaidie kuwapata mbuzi wangu kwani naamini kabisa mkuu huyu wa kituo (Neligwa), anafahamu mbuzi wangu waliko kama hahusiki asingeweza kumuachia mwizi ikiwa ni ishara ya kutaka kupoteza ushahidi,”alisema Kikwaba.
Kikwaba, alisema kwamba kuna haja ya kusaidiwa kwa vile malalamiko yake yamechukuwa zaidi ya miezi mitatu sasa bila ya kuonesha ishara yeyote ya kupatiwa haki yake kutoka kituo hicho cha polisi.
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augstino Ollomi, ili kutoa ufafanuzi, alisema kuwa anaomba kukutana na mlalamikaji huyo kwa ajili ya kusikiliza madai yake kisha aweze kuyatafutia ufumbuzi.
“Naomba nisaidie namba ya huyo mlalamikaji ili nipate kumpigia, ni msikilize ili kuona kama ni kweli hayo anayoyasema tuweze kumchukulia hatua mhusika,”alisema Kamanda Ollomi.
Hata hivyo, Kamanda Ollomi, alisema endapo Kikwaba, atabainika kuwa ametoa taarifa za uongo basi atambue kuwa polisi watamchukulia hatua za kisheria.

No comments:

Post a Comment