WASIMAMIZI wa mirathi wa familia ya marehemu Salum
Malingumu, wamemlalamikia Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Masanze, wilayani
Kilosa, Mororgoro, Shadrack Mlewa, kwa kushirikiana na mke wa marehemu, Mariam
Malingumu, kujinyakulia magari mawili kati ya matatu ya marehemu huyo kinyume cha
sheria za mirathi.
Hata hivyo, Mlewa, amesema malalamiko hayo hayana ukweli na
iwapo wasimamizi wa mirathi wameona kuna tatizo walipaswa kumlalamikia kwa
hakimu wake wa wilaya ili ikiwezekana amchukulie hatua badala ya kukimbilia
kwenye vyombo vya habari.
Mmoja wa wanafamilia hao, alisema malalamiko yanatokana na
hakimu huyo kuonekana akiwa na magari hayo mawili aina ya Hiace, akiyamiliki
kama mali yake.
Akizungumza na Tanzania Daima hivi karibuni jijini Dar es
Salaam, mwanafamilia huyo aliiomba serikali kuingilia kati mgogoro huo wa mali
za mirathi ambao umeazishwa na Mariam.
“Mlewa aliivuruga kesi hii na kufanya kila mara
kubadilishiwa mahakimu, hata hivyo tulishashinda baada ya kusikilizwa na hakimu
mwingine na hatimaye yule mama akaondolewa kwenye nafasi ya usimamizi wa
mirathi baada ya kuhamisha mali za marehemu bila ya ridhaa ya warithi wengine,”
alisema.
Mwanafamilia huyo alisema mashahidi hao pia walikiri
mahakamani kwamba mali nyingine tayari zimegawiwa kwa warithi wote, huku magari
matatu ambapo mawili ni yale yanayodaiwa kunyakuliwa na hakimu huyo bado
hayajagawanywa.
Mlewa akizungumzia tuhuma hizo, alisema kuwa ameshangazwa
na malalamiko hayo, ambayo amedai kuwa hayana ukweli wowote kwani hana magari
ya familia hiyo.
“Siwezi kuzungumzia kwa undani suala hilo, kama ni
kulizungumzia ni lazima nipewe ruhusa na kiongozi wangu ambaye ni hakimu wa
wilaya,” alisema Mlewa.
Mlewa alisema kama kuna kitu hakikuwaridhisha walipaswa
kufikisha malalamiko hayo kwa mkuu wake wa kazi au kwenye bodi ya wilaya ili
kusikilizwa, ili kubaini tatizo liko upande upi kati yao,” alisema Mlewa.
Kwa upande wake, Mariam, alikana magari hayo kuchukuliwa na
hakimu, bali wanayo wenyewe.
Alisema baada ya kusikia magari hayo yanapaswa kuuzwa ili
fedha zigawanywe, kitendo hicho kikawaudhi na kuamua kuyanyofoa vifaa vyote na
kuyaacha magari hayo kubaki kama chuma chakavu, isitoshe wao ndio wanajua
yaliko.
“Tangu amefariki dunia mume wangu nimekuwa nikiishi kwa
shida, kwani sina msaada wowote kutoka kwao wakati wanajua nimeachiwa watoto
wawili ambao wanasoma na kuhitaji msaada,” alisema Mariam.
Pia alipinga kuhusika na nyumba iliyoko Morogoro na kusema
anachofahamu nyumba hiyo wamekwisha kuiuza na sasa wanataka kumtoa kwenye
nyumba anayoishi na wadogo zake ili nayo waiuze.
CHANZO TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment