KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Saturday, 9 April 2016

ZINGIZIWA WAOMBA SHANBA KUFUTIWA HATIMILIKI

WAKAZI wa Mtaa wa Zingiziwa, Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam,  wamemeomba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kufikisha kilio chao kwa Rais John Magufuli ili aangalie uwezekano wa kulifutia hatimiliki shamba lenye kubwa wa ekari 10 ambalo Manispaa ya Ilala wameshindwa kuliendeleza.
Wakazi hao walidai shamba hilo, ambalo lilitengwa na manispaa hiyo kwa ajili ya hifadhi ya wanyama (Zoo), limetelekezwa kwa muda mrefu na hivyo kusababisha ongezeko la nyoka aina chatu ambao wamekuwa tishio kwa maisha yao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana,  wananchi hao walisema Manispaa ya Ilala ilitenga shamba hilo kama hifadhi, tangu mwaka 2005 hata hivyo, tangu kipindi hicho halijaendelezwa.
“Kutoendelezwa kwa muda mrefu kumefanya matokeo yake kiwe kichaka cha kujifichia majambazi huku baadhi  ya watu wakishambuliwa na nyoka wakali,” alisema mmoja wa wakazi hao.
Mohamed Kaunda, alisema ni wakati mwafaka kwa Rais Magufuli  kulifutia hatimiliki shamba hilo, ili lirudishwe serikalini kwa ajili ya matumizi mengine ikiwemo kuanzishwa miradi ya maendeleo kama  zahanati.
Mwenyekiti wa Mtaa huo, Ally Mkwanda, alisema katika mtaa wake wapo watu wanaomiliki ekari kuanzia tano  hadi 10 za mashamba lakini wanashindwa kuziendeleza.
 “Kikwazo kikubwa katika mtaa wangu wamiliki wa maeneo hawayafanyii usafi,  yamekuwa kichaka cha wezi na kuwa na majoka makubwa ambayo ni hatari,” alisema Mkwanda.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Isaya Mgurumi alikiri kuwepo kwa mpango wa kutengenezwa hifadhi ya wanyama  katika eneo hilo na kwamba mpango huo utaanza hivi karibuni.
Alisema katika mwaka huu wa fedha, bajeti inaonyesha Sh.Milioni 100 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi huo, hivyo kuwaomba wakazi wa eneo hilo kuondoa hofu kwani ujenzi unatarajiwa kuanza muda si mrefu toka sasa.

No comments:

Post a Comment