KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Monday, 9 March 2015

DK. MWAKYEMBE: NAWASHANGAA WANAOMWAGA POROJO ZA KISIASA

WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Harrison
Mwakyembe, amesema wabaya wake wameanza kumchafu kwa kutoa porojo za kisiasa wakimhusisha na kashfa ya mabehewa feki ya TRL.

Katika taarifa yake iliyosanbazwa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam leo, Dk Mwakyembe, alisema kuna watu ambao wamekuwa wakipeleka taarifa za uzushi kwenye vyombo vya habari zenye lengo la kumchafua hususan katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Octoba mwaka huu.

Alisema watu hao wamekuwa wakimhusisha kwenye mchakato wa zabuni ya TRL ambao kwa kawaida waziri hana mamlaka nao kikanuni na kisheria.

Dk. Mwakyembe, alisema wakati akiwa waziri mwenye dhamana  wa uchukuzi, baada ya kupokea malalamiko kuhusu mabehewa yaliyonunuliwa kutokuwa na viwango vinavyokubalika, alichukua hatua za awali za kuunda tume.

Alisema tume ilianza kazi ya kuchunguza suala hilo mara moja, ili kujiridhisha na kutafuta ukweli wa jambo hilo.

“Baada ya kupokea taarifa ya awali ya uchunguzi uliyofanywa na tume hiyo, nilichukua uamuzi wa kuiagiza Bodi ya Wakurugenzi ya TRL kuivunja Bodi ya Zabuni.

Dk. Mwakyembe alisema baada ya bodi hiyo ya zabuni kuvunjwa, aliagiza Bodi hiyo ya wakurugenzi ya TRL iwasimamishe kazi  maofisa waandamizi wote wa TRL waliyohusika katika mchakato wa manunuzi wa mabehewa hayo ili kupisha uchunguzi uliyokuwa ukiendelea kufanywa na tume.

“Niliiagiza wizara na Bodi ya wakurugenzi ya TRL kuiomba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ifanye uchunguzi wa kina wa mkasa mzima, kazi ambayo nafahamu inaendelea kufanyika hadi sasa.

“Kwa msingi huo habari zinazosambazwa kwenye vyombo vya habari na kunihusisha na kashfa ya sakata hilo imenishtua na kunishangaza kwa kuwa kama ningekuwa na husika kwa namna moja au nyingine nisingeweza kuchukua hatua nilizozieleza,”alisema Dk. Mwakyembe.

Kuhusu mabadiliko ya Baraza  la Mawaziri

Dk Mwakyembe, alisema kuhusu mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Rais Jakaya Kikwete, ambayo yamefanya ahamishiwe katika Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwamba ni kwa sababu ya kuepushwa na kadhia ya kashfa hiyo ya ununuzi wa mabehewa feki.

“Hilo ni jambo la kushangaza na uelewa mdogo wa baadhi ya waliyotoa taarifa hizo, kwa kutoelewa namna Serikali inavyofanya kazi,”alisema Dk. Mwakyembe.

Dk. Mwakyembe, alisema uamuzi wa kuhamishwa wizara, ulifanywa na Rais kwa sababu tofauti kabisa  na hizo za kusadikika zilizoandikwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari .

Alisema kama Rais aliona ana dosari, hangekuwa na sababu kabisa ya kumteua ili amsaidie kuendesha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), katika kipindi hiki ambacho nchi imepata fursa ya kuwa mwenyekiti wa Jumuiya hiyo.

No comments:

Post a Comment